Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam limejipanga kuhakikisha ulinzi unaimarishwa katika mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga.
Mchezo huo utachezwa kesho Jumamosi Desemba 11, 2021 katika uwanja wa Benjamini Mkapa lengo ni kuwafanya mashabiki wa Mpira wa miguu watakaoshuhudia mchezo huo wawe kwenye mazingira ya amani na utulivu.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro limepiga marufuku kuingia uwanjani hapo na silaha.
"Jeshi linapiga marufuku kwa mtu yeyote yule asiyehusika na mambo ya kiusalama kuingia uwanjani na silaha yoyote ikiwa ni pamoja na silaha za moto, visu, Panga au mawe kwa kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa" imeeleza taarifa hiyo.