Polisi Yasimulia Mauaji ya Muhitimu Sua, Mmoja Mbaroni



Morogoro. Kufuatia mauaji ya muhitimu wa chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) kozi ya sayansi ya mazingira, Magreth Mashuwe (22) jeshi la Polisi linamshikilia na kumuhoji mwanaume mmoja kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya muhitimu ambaye mwili wake uliokotwa kwenye mashamba ya Sua.

Akizungumzia sababu za kumshikilia mtuhumiwa huyo ambaye naye ni mhitimu wa Sua kozi ya misitu mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Morogoro kamishna msaidizi wa polisi ACP Ralph Meela amesema kuwa ni kutokana na mahusiano ya kimapenzi baina ya marehemu na mtuhumiwa ambapo siku za hivi karibuni walikuwa na kutoelewana.

Aidha mkuu huyo wa upelelezi alisema kuwa baada ya kumuhoji mtuhumiwa alidai kuwa kabla ya tukio hilo marehemu alimuaga kuwa anakwenda kihonda barabara ya mazimbu kutafuta kazi ambayo aliahidiwa na tajiri mmoja ambaye hakuweza kumfahamu.

"Kutokana na hilo tunamashaka na mtuhumiwa huyu kwa sababu yeye kama ni mpenzi wake ambaye walikuwa wakiishi chumba kimoja kama mke na mume kwa nini hakupata wasiwasi baada ya kuona mpenzi wake hajarudi, mpaka tulipomkamata ndio anatueleza hayo," alihoji Meela.


Alisema kuwa pamoja na mashaka hayo lakini zipo sababu nyingine ambazo zinafanya jeshi la Polisi limshikilie ikiwa ni pamoja na hali ya mahusiano yao kwa siku chache zilizopitaka kabla mauaji hayo.

Mkuu huyo wa upelelezi alisema kuwa pamoja maelezo hayo lakini bado Polisi wanendelea na uchunguzi na kwamba uchunguzi wa kidaktari ulibaini kuwa muhitimu huyo alivunjwa shingo.

Mwili wa muhitimu huyo uliokotwa Desemba 14 baada ya kuonekana na msamalia mwema ambaye baadaye alitoa taarifa polisi.


Mwili wa marehemu huyo umeshakabidhiwa kwa wazazi wake kwa ajili ya mazishi.

Kwa upande wake Makamu mkuu wa chuo cha Sokoine cha Kilimo (Sua) Profesa Raphael Chibunda alikiri kwamba marehemu ni muhitimu wa Sua hata hivyo alisema kuwa uongozi na wanajamii wa Sua wamepokea kwa masikitiko makubwa mauaji hayo na kulaani vikali.

Hata hivyo alitoa wito kwa wanafunzi kuacha tabia ambazo zinaweza kiwaweka kwenye hatari badala yake waishi kama wanafunzi.

"Kwa sasa tunaliachia jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi zaidi na wao ndio wenye mamlaka ya kusema nini chanzo chanzo cha mauaji haya, na kama kuna waliohusika basi wachukuliwe hatua za kisheria lakini kiukweli kama chuo tumehudhunika," alisema Profesa Chibunda.


Aliwashauri wanafunzi waliohitibu kuendelea kuishi mikononi mwa wazazi huku wakiendelea kutafuta ajira ili waweze kuepukana na hatari zinazoweza kuwapata kwa kukaa nje ya wazazi ambao sio sehemu salama.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad