Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemuaomba Rais Samia suluhu Hassan kuharakisha mabadiliko madogo ya Katiba ili kuruhusu kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 26/2021, ikiwa siku chache zimepita tangu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuteua kikosi kazi kitakachoandaa vizuri maazimio 80 ya kongamano lilofanyika Dodoma na kuyawasilisha kwenye Baraza hilo ndani ya mwezi mmoja kuyarekebisha na kuwasilisha kwa Rais Samia kuyatekeleza.
Akizungumza Dar es Salaam,Jana Mwenyekiti huyo amesema mabadiliko hayo ni pamoja na sheria ya uchaguzi itungwe upya kukidhi mahitaji ya tume hiyo ili iwezi kusimamia chaguzi zinazofanyika kwa haki pamoja na kuipa muda wa kujipanga na uchaguzi mkuu ujao.
“Tunamuomba Rais ni vyema akafanya mabadiliko madogo ya Katiba kuruhusu kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi itungwe upya kukidhi mahitaji ya tume hiyo kufanya hivyo kutasaidia chaguzi zinazokuja kufanyika kwa haki pamoja na kuipa tume hiyo muda wa kutosha wa kuandaa uchaguzi mkuu ujao,”amesema Profesa Lipumba
Amesema kufanya mabadiliko hayo kutakuwa na manufaa makubwa ikiwemo kupitisha baadhi ya mambo waliyokubalina kati ya wananchama wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete ikiwemo ushindi wa Rais kupata kura zaidi ya asilimia 50 ya kura halali na matokeo ya Rais yaweze kuhojiwa Mahakamani.
Profesa Lipumba katika maelezo yake amebainisha kwamba ni kweli wanahitaji la mchakato wa Katiba mpya ambayo itakuja kumaliza baadhi ya matatizo lakini hata hivyo wanaona mchakato huo unaweza kuchukua muda mrefu jambo ambalo halitaleta tija kidemokrasia nchini.
“Kwakuwa muafaka wakitaifa umefanyika licha ya kwamba baadhi ya vyama vilisusia ni vizuri tukatumia fursa hii katika kipindi ambacho Rais ameshafungua milango tufanye mabadiliko madogo chaguzi zifanyike kwa uhuru wakati tunaendelea kusubiri mchakato wa katiba mpya,”amesema Profesa Lipumba.