Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro amesema kwamba hatampa chanjo bintiye mwenye umri wa miaka 11 dhidi ya COVID-19.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa msimamo wake hasi, wa kupinga chanjo, ambao umekosolewa na wataalam wa afya ya umma, na hata kuathiri ufuasi wake wa kisiasa.
Kiongozi huyo wa mrengo wa kulia aliongeza kuwa waziri wa afya wa taifa hilo, Marcelo Queiroga, ataeleza hapo Januari 5 mwakani, jinsi ambavyo Brazil itaendesha kampeni yake ya chanjo dhidi ya corona, kwa watoto wa miaka 5 hadi 11, ambayo iliidhinishwa mapema mwezi huu.
"Watoto wamekuwa hawafi kwa njia ambayo inahalalisha chanjo kwa watoto," aliwaambia waandishi wa habari katika jimbo la Kusini la Santa Catarina.
Utoaji wa chanjo kwa watoto imekuwa mada yenye utata nchini Brazil, ambapo wafuasi wakuu wa Bolsonaro, wamepinga kwa dhati hatua hiyo, hata kama idadi kubwa ya watu, kwa jumla wanaunga mkono utoaji wa chanjo.