Dar es Salaam. Hali ni tete, ndivyo unavyoweza kueleza baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza kuzivunja Bodi ya Mamlaka ya Badari Tanzania (TPA) na ile ya Shirika la Meli kwa kuwaondoa wenyeviti wake baada ya kutoridhika na utendaji kazi wao.
Pia, ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi baada ya kunusa harufu ya ufisadi ikiwemo baadhi ya kampuni kulipwa fedha kwa ajili ya kutengeneza mifumo, lakini kazi haikufanyika.
Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari inaundwa na mwenyekiti wake Profesa Ignas Rubaratuka huku Makamu wake akiwa Dk Delphine Magere. Wajumbe ni Malata Pascal, Dk Jabiri Bakari, Masanja Kadogosa, Jayne Nyimbo, Mhandisi Ephrem Kirenga na Eric Hamissi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Bandari.
Akizungumza leo Jumamosi Desemba 4,2021 wakati akizindua gati katika Bandari ya Dar es Salaam. Huku akionyesha kufahamu mambo mengi yanayoendelea ndani ya taasisi hizo, Rais Samia amesema kuna madudu mengi yanayofanywa ndani ya mamlaka hizo.
Amesema licha ya baadhi ya madudu hayo kuonyeshwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
Rais Samia amesema bado kuna mianya ya uvujaji wa mapato katika mamlaka kutokana na mifumo ya malipo kuchezewa na wafanyakazi.
“Mkurugenzi nimekuleta hapa kusimamia bandari, Takukuru naomba, naagiza, natoa amri uchukue hatua dhidi ya watu hawa haraka sana na kama ripoti hiyo hamna nitawapatia ya nini kilichofanyika hapa. Watu waliofanya hayo wapo bado ofisini…watu tunachekeana tu, tunatizamana tu. Watu wapo maofisini wanaendeleza wizi na ubadhirifu wa mali za umma.
“Mifumo imekuwa ikichezewa, inaonyesha kuwa mizigo imelipiwa kutoka getini, lakini sio kweli haijalipiwa hivyo bandari kukosa mapato. Haya mapato yanayoonekana leo hayakupaswa kuwa hivyo yalivyo. Kama tungechukua hatua kudhibiti wizi huu tungekuwa mbali sana kwenye kukusanya mapato,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Nimepata fursa ya kupitia ripoti ya ukaguzi maalumu ya mfumo wa mapato, ndani ya ripoti niliona fedha nyingi zilizotumika kuajiri kampuni za kufunga mifumo ya kielektroniki ambayo haikushirikisha mamlaka zingine za Serikali. Ipo kampuni iliingia mkataba wa Sh694 milioni na ililipwa Sh600 milioni lakini haikumaliza kazi iliyotakiwa na mkataba ukavunjwa. Fedha zilikwenda bila kazi kufanywa. Ripoti pia ilieleza kuwa utaratibu wa kutoa zabuni hizo haukufuatwa,” ameongeza Rais Samia.
Rais Samia amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Eric Hamissi kusimamia na kudhibiti mapato ya mamlaka hiyo kwani, mambo yote hayo yanatokea wakati Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari ipo, lakini hakuna hatua imechukua.
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia amemtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kushughulikia mambo hayo ama amweleze kama ameshindwa ili aone nini atafanya ikiwemo kuteua waziri mwingine atakayeweza kumsaidia.