Sababu za watu kuumwa mafua, kifua zatajwa


Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watu kwa takriban wiki moja sasa wakiwa na hofu kutokana na kuugua kikohozi kikali, mafua, maumivu ya kichwa, mgongo na homa, Serikali imesema hali hiyo ni ya kawaida kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, (mvua) zinazoendelea kunyesha maeneo tofauti.

Hata hivyo, baadhi ya madaktari wameliambia Mwananchi kuwa ni vema watu wachukue tahadhari zilizotolewa dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

Desemba mwaka jana liliibuka wimbi la tatu la virusi vya Uviko-19 vilivyojulikana kama Delta na watu kadhaa duniani walifariki dunia, huku wengine wakiugua.

Hofu ya wimbi hilo kuingia hapa nchini iliondolewa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyewahakikishia Watanzania kuwa virusi hivyo bado havijaingia nchini na kushauri watu waendelee kujikinga.


 
Akizungumza na Mwananchi, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Aga Khan, Alex Masao alikiri kuhudumia wagonjwa wengi wenye dalili hizo kwa takribani wiki mbili sasa.

“Tunapokea wagonjwa wengi wiki hii na kwa kifupi tu kati ya wagonjwa 10 tunaowapokea Aga Khan sasa hivi, sita wanakuja na malalamiko ya homa, mafua, kifua, kuchoka na maumivu ya mwili,” alisema.

Dk Alex alisema umefika wakati sasa kila mtu anaumwa na ni wachache wanaofika vituo vya afya kwa kuwa utamaduni wa kuishughulikia afya si wetu Tanzania. “Mtu anakuwa hajali lakini analalamika kupata maumivu ya mwili.”

Alisema baada ya kufanya vipimo kwa wagonjwa walio wengi amebaini kuwa ni maambukizo yanayotokana na kirusi ambacho hakuwa tayari kukizungumzia.

“Haya ni maambukizi yaliyotokana na kirusi ambayo yanaambukiza kwa wengi zaidi kwa sasa. Bado hatuwezi kusema ni kirusi gani kwa kuwa hatujakifanyia uchunguzi maabara, inachukua muda mrefu, ila hili ni wimbi la nne limekuja kistaarabu hivyo watu wafuate kanuni za kujilinda.”

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati alisema kuibuka kwa matatizo hayo huenda kumetokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Hali ya hewa inavyobadilika kidogo, kunakuwa na mabadiliko makubwa kwa virusi vidogo vidogo na vipo vingi sana na vinabadilika kulingana na mazingira yanavyobadilika.”


 
Alisema wagonjwa wanaopata maudhi hayo hata wakichukuliwa vipimo vya maabara hawakutwi na malaria wala magonjwa mengine.

Alisema magonjwa hayo yamekuwa yakiwapata watu wengi wanaoishi jijini Dar es Salaam kwa kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zinasababisha mabadiliko kwa wadudu wanaobadilisha protini chache hivyo wakiingia mwilini, mwili unashtuka na kuona ni kitu kipya.

Hata hivyo, Dk Osati alisema mara nyingi homa hiyo hupona yenyewe, “mwili unatengeneza kinga ya haraka dhidi yao mwili unatulia.”

Nini ufanye?

Dk Osati alisema kitu cha kwanza kwa mtu atakayehisi mabadiliko katika mwili ni kufika hospitali kwa ajili ya vipimo ili kujua iwapo wana maambukizi ya magonjwa mengine au la.

Alisema mgonjwa akiripoti hospitali itasaidia kubaini iwapo ni homa hiyo au amepata maambukizi ya Uviko-19, kama sivyo utaambiwa nini cha kufanya sambamba na kupatiwa dawa ya kupunguza maumivu, dawa ya kikohozi, ushauri pia wa kunywa maji ya kutosha mara nyingi tunawashauri hivyo.

Dk Osati alishauri kuwa hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa, hasa za vipimo vya maabara na kwamba tahadhari ni muhimu kwa kuwa mlipuko wa Uviko-19 umekuwa ukitokea nchini Kati ya Desemba na Julai.

Baadhi ya wafamasia walilalamikia wagonjwa kuhitaji dawa za kuwatibu pasipo kwenda kupima ilhali wanaonyesha dalili za maambukizi ya magonjwa mengine. Jimmy Bujeni ambaye ni mhudumu wa famasi alisema amepokea wagonjwa wengi wakienda kwa ajili ya homa, mafua, mafindofindo na kukohoa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros alisema kirusi omicron kinasambaa kwa kasi kuliko kirusi kingine chochote cha Uviko huku akisema hadi sasa kimefika kwenye nchi 77.

Nchini Kenya, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe alisema: “Tumegundua virusi vya omicron miongoni mwa wasafiri watatu ambao tayari wameshatengwa na kuna dalili vimeenea ulimwenguni kote”.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad