Sabaya alivyotumia milioni 90/- anazodaiwa kuzipata kwa rushwa




Sabaya alivyotumia milioni 90/- anazodaiwa kuzipata kwa rushwa
SHAHIDI wa 13 katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, Ramadhani Juma (39) amedai mahakamani kuwa Sabaya alipochukua rushwa ya Sh milioni 90 alianza kula na kunywa na wenzake.

Shahidi huyo amedai eneo ambalo mshtakiwa huyo na wenzake walienda kula kuwa ni Aim Shopping Mall iliyopo karibu na ofisi za Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na baadaye saa 2:00 usiku walikuwa Tulia Lodge Sakini, jijini Arusha.

Juma ambaye alikuwa Kiongozi Mkuu wa Kikosi kazi cha Upelelezi kilichoshirikisha makachero wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi Kituo Kikuu cha Polisi Arusha alidai hayo wakati akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa serikali, Felix Kwetukia mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda.

Shahidi huyo alidai kuwa katika uchunguzi na upelelezi wa awali ulioshirikisha baadhi ya watuhumiwa akiwemo John Odemba mshitakiwa wa nne katika kesi hiyo, Jackson Macha, mshitakiwa wa sita na Nathani Msuya na mshitakiwa wa saba walikiri kutumwa na Sabaya na walimpelekea rushwa ya Sh milioni 90 akiwa Aim Shopping Mall alipokuwa akiwasubiri.


 
Alidai kuwa watuhumiwa hao walikiri na kueleza kuwa walipewa chakula na vinywaji hapo Aim Shopping Mall na baada ya kazi hiyo saa 2:00 usiku walipelekwa katika Lodge ya Tulia iliyopo Sakina ndani ya Jiji la Arusha. Shahidi huyo alidai watuhumiwa hao walieleza mgao wa fedha ulivyotolewa na Sabaya baada ya kukabidhiwa na kuweka fedha hizo zilizokuwa katika boksi kwenye buti ya gari ya serikali STL 5434.

Alisema katika mgao huo, John Odemba alipewa Sh 300,000 na Sadiq Kiiza ambaye hayupo katika mashtaka hayo alipewa Sh 450,000. Wengine waliopewa mgao wa Sh milioni 90 ni mshitakiwa wa saba Msuya aliyepewa Sh 500,000, mshitakiwa wa tatu, Watson Mwahomange Sh 600,000, mshitakiwa wa pili, Enock Mnkeni Sh milioni 1.5, Slyvester Nyegu mshitakiwa wa tano Sh milioni 2.2 na Macha, mshitakiwa wa sita Sh milioni 1.4.

Alidai kuwa katika uchunguzi wao na taarifa za baadhi ya watuhumiwa walibaini kuwa Sabaya alikodisha chumba Tulia Lodge na siku hiyo ya Januari 22, mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku alimwamuru dereva wake akaegeshe gari ya serikali na dereva alifanya hivyo. Alidai katika uchunguzi na upelelezi wao waligundua kuwa Mrosso alikwenda benki ya CRDB Tawi la Kwa Mrombo akiwa chini ya ulinzi wa vijana wa Sabaya, Macha, Msuya na Odemba na kutoa pesa hizo, Sh milioni 90.


Juma alidai waligundua hilo kupitia benk slip ya kutoa ya CRDB ya Januari 22, mwaka huu na taarifa ya akaunti ya Mrosso vyote alipewa na meneja wa benki hiyo ikiwa ni sehemu ya nyaraka katika kesi hiyo ambavyo vimepokelewa kama vielelezo katika kesi hiyo. Hata hivyo, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mosses Mahuna walipinga shahidi huyo kuichambua video ya CCTV Camera ya CRDB kwa Mrombo kwa madai kuwa yeye sio mtaalamu.

Hakimu aliahirisha kesi hadi Desemba 29 mwaka huu atakapotoa uamuzi mdogo kuhusu video hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad