Babati. Sakata la kukamatwa na polisi na kulazwa mahabusu kwa viongozi wawili wa CCM wilayani Babati Mkoa wa Manyara, kwa madai ya kumpiga askari Polisi limechukua sura mpya baada ya mashuhuda wa tukio hilo kudai kuwa polisi huyo hakupigwa.
Viongozi waliokamatwa na kulazwa mahabusu katika kituo cha Kiru wilayani humo, ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Babati, Filbert Mdaki (52) na Katibu wa UVCCM Wilaya hiyo George Sanka (46), ambapo inadaiwa kuwa walimpiga mateke na fimbo Koplo Baraka aliyekuwa akihoji sababu ya mkusanyiko wa wanachama wa chama hicho Desemba 16.
Mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo Amos Bura akizungumza leo Desemba 22, amesema viongozi hao hawakupaswa kukamatwa na kulazwa mahabusu kwani hawakumpiga askari.
Bura amesema viongozi hao walikuwa kwenye mkutano wa mgogoro wa ardhi wa Kijiji cha Kirudiki na mwekezaji ndipo askari huyo akataka kuwepo mkutano hapo.
"Viongozi hao wawili walikuwa wanatumia lugha ya kidiplomasia katika kumsihi huyo askari aondoke kwenye mkutano wao na siyo kumpiga," amesema Bura.
Akizungumzia juu ya tukio hilo, katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), George Sanka amesema wao hawakumpiga askari polisi kama inavyozungumzwa, ila walikuwa wanazungumza naye ili aondoke kwenye eneo hilo baada ya watu kujawa hofu baada ya kumwona.
Hata hivyo, katibu wa CCM Wilaya ya Babati Vijijini, Filbert Mdaki amesema hayupo tayari kuzungumza kwenye vyombo vya habari juu ya tukio hilo.
Akizungumzia maoni ya wana CCM hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Benjamin Kuzaga amesisitiza kuwa askari huyo alipigwa na bado wako kwenye uchunguzi wa suala hilo.