RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo mahususi kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kusikiliza na kutatua malalamiko yatokanayo na unyanyapaa wa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU).
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais alisema hatua ya kuwasikiliza Waviu inalenga kuimarisha mwitikio wa mapambano dhidi ya Ukimwi nchini.
Majaliwa alimwakilisha Rais Samia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika jijini Mbeya jana na kubeba kaulimbiu isemayo; ‘Zingatia Usawa. Tokomeza Ukimwi. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.’
Rais aliitaka pia Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Afya kuja na mikakati mizuri ya kutunisha Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi nchini ili uanze kujitegemea badala ya kutegemea ufadhili wa fedha kutoka nje.
Alibainisha kwamba maambukizi mapya ya VVU yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi kufikia 68,000 mwaka jana.
Rais pia kupitia kwa Waziri Mkuu aliitaka Wizara ya Afya kujenga vituo vya vijana walau kimoja katika kila kanda ili kuwajengea uwezo, ujuzi, stadi za maisha na kuwawezesha kiuchumi waathirika wa dawa za kulevya na wasichana balehe na wanawake vijana.
Alishauri mwongozo wa unasihi usambazwe kwenye shule zote ili utoaji wa huduma hiyo uzingatiwe katika shule zote.
Pia aliitaka TACAIDS kuhakikisha mikakati ya kitaifa na kisekta ya kudhibiti Ukimwi inazingatia na kukidhi takwa la mazingira ya nchi hii, huku sekta binafsi na za umma zikitakiwa kuhamasishwa na kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya vifaa na bidhaa tiba za ugonjwa huo hapa nchini ili kupunguza gharama za kuagiza kutoka nje.
Rais pia aliitaka Wizara kujikita kwenye uwekezaji wa kinga msingi nchini na kuyafikia makundi yaliyopo kwenye hatari zaidi ya maambukizi mapya ya VVU wakiwemo vijana, wavuvi, madereva wa masafa marefu na wachimbaji wa madini.
“Mwaka 2015 tulianzisha Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi, tumekuwa tukihamasisha uchangiaji wa mfuko kwa njia mbalimbali. Tayari mfuko umeanza kufanya kazi, baadhi ya maeneo ambayo mfuko huo umeyafadhili ni kugharamia ununuzi wa dawa za kutibu magonjwa nyemelezi kwa ajili ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, mfuko pia umegharamia afua za kutoa elimu na kuhamasisha utoaji wa huduma hasa vyuo vikuu na vya kati,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutenga bajeti na kutafuta vyanzo endelevu vya kutunisha mfuko huu kadri uchumi utakavyoruhusu.
“Natoa agizo kwa TACAIDS kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Afya, kuangalia utaratibu mzuri na wa uhakika wa kutunisha mfuko huu ili tuanze kujitegemea wenyewe. Mfuko huu ukiimarika utasaidia sana kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje,” alisema.
Mafanikio vita dhidi ya Ukimwi
Alisema kumekuwa na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa miaka 38 sasa tangu uingie hapa nchini na miaka 40 tangu uingie duniani.
Aliyataja mafanikio hayo hapa nchini kuwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha upimaji cha watu wenye VVU kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019, kuongeza kiwango cha Waviu wanaopata dawa za kufubaza VVU (ARV) kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 98 mwaka 2019.
Mafanikio mengine alisema ni kuongeza kiwango cha kufubaza kwa Waviu wanaotumia dawa kutoka asilimia 87 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 92 mwaka 2019, kupunguza vifo vinavyotokana na Ukimwi kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi kufikia vifo 32,000 mwaka jana, kushusha idadi ya maambukizi mapya ya VVU kutoka watu 110,000 mwaka 2010 hadi kufikia 68,000 mwaka jana.
Majaliwa pia alisema kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kimepungua pia kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia saba mwaka jana.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaowanyanyapaa na kuwabagua watu wanaoishi na VVU wakiwemo watumishi wa afya ikiwemo kuvujisha siri za wagonjwa.