Samia "Machinga hamtajuta, Naomba Mtuamini Mtupe Muda"




RAIS Samia Suluhu Hassan amesema machinga hawatajutia uamuzi wa serikali wa kuwahamishia kwenye maeneo maalumu, akiahidi kuwa mambo mazuri yanafuata kwa wafanyabiashara wadogo hao.

Aliitoa ahadi hiyo jana mbele ya wananchi wakati akiwa eneo la Vikundi wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Rais Samia alisema kuwa suala la machinga ni lake na kuwaomba wampe muda, akisisitiza kuwa hawatajuta kwa kuwa atahakikisha wanajiajiri sehemu nzuri zenye huduma zote.

Mkuu wa nchi alikwenda Mkuranga kuzindua kiwanda cha kutengeneza nyaya za mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing na alipofika Vikindu alisimama na kutoa ahadi hiyo kwa machinga.

“Nimeona vidole vya vijana vipo juu, nadhani wanataka kuzungumzia suala la machinga, hilo suala ni langu, ni mradi wangu binafsi na hilo ninataka kuwaahidi mazuri kwenye hilo.


 
“Nipeni muda, kubalini ya sasa hivi, hameni, nendeni mnakopangishwa, ninataka kuwaahidi kwamba hamtajuta, mimi na halmashauri tutafanya kazi kuhakikisha vijana wetu wanajiajiri sehemu nzuri, sehemu zenye huduma zote, wanafanya kazi saa 24 kwa wale watakaoweza, hamtajuta ndugu zangu," alisisitiza.

Rais Samia alisema upo mradi mkubwa ambao kwa sasa anazungumza na ulimwengu ili kuzikopesha halmashauri moja kwa moja na hizo fedha zitatumika kujenga maeneo ya machinga.

“Ninaomba mniamini, ninaomba mniachie, tupeni muda tulifanyie kazi, mambo yatakuwa mazuri,” Rais alisema.


Akizindua kiwanda hicho cha nyaya, Rais Samia alisema serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, hivyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya kufanyia biashara na uwekezaji.

Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza Tanzania na kuwahakikishia usalama wa mitaji yao pamoja na uhakika wa kutengeneza faida.

Rais alimpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho, Ramadhani Mlanzi, ambaye ni mzawa kwa kuona Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza.

Alisema uzinduzi wa kiwanda hicho unathibitisha uwezo na fursa nyingi ambazo nchi imejaliwa kuwa nazo ili zitumike kukuza uchumi, kuleta ajira hususan kwa vijana na kuzalisha bidhaa ambazo siyo lazima kuagizwa nje.


 
Rais Samia aliziagiza taasisi zote za serikali zinazotoa huduma katika sekya ya uwekezaji, kuondoa urasimu ambao unasababisha kupoteza baadhi ya wawekezaji waliokuwa na nia ya kuwekeza Tanzania.

Alisema serikali itaimarisha jitihada za mageuzi ya kisera na kisheria ikiwamo utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara.

Pia alimtaka Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho kukamilisha azma yake ya kujenga kiwanda cha kuzalisha simu janja ambacho uwapo wake utachangia ajira kwa vijana.

Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha kiasi cha kilometa 24,000 za Optic fiber kwa mwaka na kinatarajiwa kutoa ajira zipatazo 670 kitakapokamilika katika awamu zote, hivyo kukifanya kuwa kiwanda cha tatu kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza Afrika Mashariki na Kati.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad