Dar es Salaam. Mahakama Kuu imekataa ombi la Serikali kutaka ipewe kibali cha kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama hiyo uliotengua hukumu ya Kamati ya Mawakili kumvua uwakili Wakili Mwandamizi Fatma Karume.
Jaji Stephen Magoiga amelikataa ombi hilo baada ya kuridhika kuwa sababu za Serikali kuomba kibali cha kukata rufaa hiyo hazikuwa na mashiko.
Jaji Magoiga amesema katika uamuzi wake kuwa baada ya kutafakari hoja za pande zote, kiapo na kiapo kinzani pamoja na kesi rejea amebaini utolewaji wa kibali cha kukata rufaa si jambo la moja kwa moja.
Amesema licha ya Serikali kukidhi vigezo na utaratibu wote wa kuomba kibali hicho, imeshindwa kuishawishi mahakama kuwa ilikuwa na hoja za msingi zilizopaswa kuamriwa na Mahakama ya Rufani.
Uamuzi wa mahakama ni ushindi kwa Karume ambaye katika miaka ya hivi karibuni amejibainisha kama mtetezi wa haki za binadamu na mkosoaji mkubwa wa sera za Serikali.
Karume ambaye amewahi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) aliondolewa katika orodha ya mawakili Septemba 23 mwaka jana baada ya Kamati ya Mawakili kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya taaluma hiyo.
Kamati ilifanya uamuzi huo kufuatia malalamiko iliyopelekewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliyemlalamikia Karume kuwa alikiuka maadili ya uwakili kwa kutoa lugha chafu dhidi yake wakati wa usikilizwaji wa kesi ya kikatiba aliyokuwa akiisimamia mbele ya Jaji Kiongozi wa wakati huo, Eliezer Feleshi.
Karume kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga kuvuliwa uwakili.
Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa Juni 17 na jopo la majaji watatu ambao ni Issa Maige, Dk Deo Nangela na Edwin Kakolaki ilibatilisha uamuzi wa kamati hiyo ya mawakili.
Majaji hao, pamoja na mambo mengine, walikubaliana na Karume kuwa Kamati ya Maadili haikuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ilisema kwa kusikiliza na kuamua shauri hilo, kamati hiyo ilikwenda kinyume na amri ya Jaji Kiongozi ambaye alimsimamisha tu kwa muda Karume kusubiri Msajili wa Mahakama Kuu awasilishe malalamiko dhidi yake katika kamati hiyo kwa mujibu wa utaratibu.
Hivyo, mahakama hiyo ilibatilisha uamuzi huo Kamati ya Mawakii ikisema AG hakuwa na haki ya kuwasilisha malalamiko hayo ambayo Jaji Kiongozi alielekeza Msajili wa Mahakama Kuu ndiye ayawasilishe kwenye kamati ya maadili.
Serikali haikuridhishwa na hukumu hiyo ndipo AG akaamua kuwasilisha Mahakama Kuu taarifa ya kusudio la kukata rufaa na maombi ya kibali cha kukata rufaa Mahakama ya Rufani, kupinga hukumu hiyo.
Akitoa uamuzi wa maombi hayo Ijumaa iliyopita, Jaji Magoiga alisema hoja ambazo mahakama hiyo inaweza kuzizingatia katika kutoa au kutokutoa kibali lazima ziwe zilizoamriwa na Mahakama Kuu.
Alisisitiza kuwa maombi ya kibali yanafungwa kwenye masuala yaliyoko kwenye uamuzi unaopingwa na si vinginevyo na kwamba, baada ya kupitia hukumu ya Mahakama Kuu amebaini hoja tatu za Serikali ni mpya (siyo sehemu ya hukumu hiyo).
Hivyo, alisema masuala hayo hayawezi kuwa msingi wa kutoa kibali cha kukata rufaa na hoja nyingine zilizotolewa na Serikali haziibui masuala yanayopaswa kuamuriwa na Mahakama ya Rufani.
“Kwa sababu zilizotolewa hapo juu mahakama hii inakataa kutoa kibali cha kukata rufaa Mahakama ya Rufani kama ilivyoombwa kwa mwombaji kushindwa kuthibitisha kuwapo kesi au hoja kwa Mahakama ya Rufani kuzitafakari,” alisema Jaji Magoiga.
Sababu za Karume kufutwa
Fatuma alilalamikiwa kukiuka maadili wakati akiwasilisha hoja zake katika kesi iliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu dhidi ya AG. Karume alikuwa akimwakilisha Shaibu katika kesi hiyo.
Ilielezwa kuwa wakati wa uwasilishaji wa hoja Karume alitumia maneno ambayo hayakuwa mazuri na si ya heshima kwa AG.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji Kiongozi wa wakati huo, Feleshi, Shaibu alikuwa akihoji uteuzi wa AG akidai kuwa kikatiba hakustahili kuteuliwa na akaenda mahakamani kumlalamikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na AG.
Karume alidaiwa kutumia lugha ya kejeli dhidi ya AG, mahakama na Wakili Mkuu wa Serikali kuwa AG bado ni junior (mchanga kisheria), na hana uwezo wa kubeba jukumu la Uanasheria Mkuu wa Serikali na kwamba amekuwa akiipotosha Serikali katika mambo mengi.
Kwa sababu hiyo, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliwasilisha Mahakama Kuu malalamiko juu ya kauli ya Karume ikidai kauli hizo ni kinyume na kanuni za mawakili zinazosimamia maadili ya mawakili na kwamba maneno hayo ya kejeli na kashfa yaliidhalilisha ofisi ya AG.
Baada ya malalamiko hayo kufunguliwa mahakamani, Jaji Kiongozi alimsimamisha Karume uwakili kwa muda na akamwelekeza Msajili wa Mahakama Kuu kuwasilisha malalamiko hayo kwa Kamati ya Mawakili.
Kinyume na maelekezo hayo ya jaji, AG wa wakati huo Profesa Kilangi aliamua kuwasilisha malalamiko hayo katika kamati hiyo.