Serikali yatoa tamko Mtanzania kukutwa kirusi kipya



 
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu kuwapo kwa taarifa za Mtanzania kupatikana na aina mpya ya kirusi cha corona kiitwacho Omicron, ikisema haijabainika iwapo mtu huyo alipatia maambukizi hapa nchini au la.

Pia imesema Maabara Kuu ya Taifa, imeendelea kusimamia upimaji wa ugonjwa wa Uviko-19 pamoja na kuangalia anuwai mpya zinazosababishwa na mabadiliko ya mara kwa mara ikiwamo kirusi cha Omicron.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi, aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa hizo ambazo zilisambaa nchini kupitia mitandao ya jamii na kuanza kuleta hofu miongoni mwa wananchi.

“Hivi karibuni kumetokea unuwai mpya ijulikanayo kama Omicron (B.1.1.529) iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza Afrika ya Kusini na Botswana. Leo (jana), tumepokea taarifa iliyoripotiwa na vyombo vya habari vya India na kuenea katika mitandao ya kijamii na kueleza kuwa India wamegundua abiria mmoja anayerudi nyumbani (India) mwenye anuwai mpya Omicron, ametokea Tanzania.

“Hata hivyo haijajulikana kama abiria huyu alitokea Tanzania moja kwa moja au alipita Tanzania kuelekea India. Pia haijulikani alipita wapi kabla ya kufika India. Kutokana na taarifa hizo, Wizara ya Afya, imeanza kufuatilia kupitia vyombo vyetu vya ndani kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini India, ili kubaini ukweli wa jambo hili na baadaye kuchukua hatua stahili,” alisema Prof. Makubi.


 
Alibainisha kwamba, wananchi waondoe hofu kutokana na habari hizo, bali kuendelea kuwa watulivu na kufanya shughuli za maendeleo kama kawaida, huku wakichukua tahadhari zote, kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kuvaa barakoa na kujiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na kufuata miongozo ya wizara kuhusu kupambana na Uviko-19.

Prof. Makubi alisema, wizara inachukua hatua zaidi za kuepusha nchi isiingie kwenye mlipuko wa nne kwa kufanya upimaji kwenye mipaka na viwanja vya ndege kwa watu wote wanaosafiri kwenda nje ya nchi.

“Wasafiri wanaogundulika hawana maambukizi ya Uviko-19 kwa kutumia kipimo cha RT-PCR hupewa cheti kuwaruhusu kusafiri. Wasafiri wanaogundulika kuwa na maambukizi huunganishwa na daktari/hospitali, ili waanze matibabu na kuwa katika uangalizi maalumu na kufuatiliwa kupitia mawasiliano yake.


“Maabara ya taifa pia imekuwa ikichunguza mabadiliko ya kirusi, kuangalia uwapo wa anuwai mbalimbali zinazotokana na mabadiliko mapya ya Omicron. Tunaomba kuwatoa wasiwasi Watanzania wote mpaka sasa hatujabaini anuwai mpya, Omicron,” alisema Prof. Makubi.

Aidha, Prof Makubi, aliagiza viogozi wote wa mikoa na wilaya, kuweka na kukagua miundombinu hasa sabuni na maji ya kunawa mikono sehemu za mikusanyiko ili kujikinga, bila kusubiri athari kubwa.

“Tunawahimiza wananchi kujitokeza kuchanja ili kujikinga na UVIKO-19 na kuanzia Desemba 7, mwaka huu, tutakuwa na kampeni maalumu za elimu za kuhamasisha wananchi wengi zaidi wajitokeze kuchanja katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu.

“Kampeni hizo zitafanyika katika ngazi za mitaa, masoko, viwanja vya mipira, stendi za basi/daladala, vyuo na kwenye taasisi mbalimbali. Nawaomba viongozi wote katika mikoa, wilaya, mitaa na vijiji, tusimamie zoezi hili kwa ufanisi,” alisema.i
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad