Shahidi "Sabaya Alitambulika Kwa Jina la Jenerali, Walikuwa Watu Hatari Sana"



Arusha.Shahidi wa 13, Ramadhan Juma (39) amedai kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na vijana wake walitumia majina bandia walipokuwa wanatekeleza matukio ya kihalifu.

Alidai kuwa, kupitia uchunguzi wake, alibaini Sabaya alikuwa akiratibu genge hilo la uhalifu huku akitambuka kwa jina la Jenerali.

Juma ambaye pia ni ofisa uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Arusha, alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo, shahidi huyo alitoa madai hayo akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Felix Kwetukia.


Alidai Machi 8, mwaka huu akiwa ofisini kwake, aliitwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, aliyemkabidhi jalada kutoka polisi ili alifanyie uchunguzi.

Aliieleza Mahakama kuwa, jalada hilo lilikuwa linahusiana na tuhuma za kuomba na kupokea rushwa, matumizi mabaya ya madaraka yaliyofanywa na Sabaya dhidi ya mfanyabiashara Francis Mrosso.

Shahidi huyo alisema wakati anafanya uchunguzi wa jalada hilo kupitia taarifa fiche alibaini Sabaya alishiriki kufanya tukio hilo akiwa na genge la vijana wake ambao ni John Odemba, Sylvester Nyegu, Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, Nathan Msuya, Jackson Macha na Sadick Kiiza.


“Taarifa fiche nilizoendelea kukusanya nilibaini Sabaya alikuwa anaratibu genge la kihalifu na wakati wanatekeleza uhalifu walikuwa wakificha uhalisia wao kwa kutumia majina bandia,” alidai shahidi huyo.

“Nilibaini Sabaya ni Jenerali, Nyegu (Kicheche), Mkeni (Dikidiki), Watson (Malimungu), Odemba (Mike one), Msuya (Chesa), Macha (Folio B) na Kiiza (Kiiza Besigye).”

Shahidi huyo alidai kuwa jalada hilo la malalamiko la Mrosso lilikuwa ndani yake na barua ya polisi ya Machi tatu ya mwaka huu ya kuhamisha jalada hilo kutoka Polisi kwenda Takukuru ili waendelee na upelelezi kuhusu malalamiko hayo.

Shahidi aliieleza Mahakama kuwa aliendelea kukusanya taarifa na alibaini Sabaya na vijana wake walikuwa wakitumia silaha za moto, ikiwamo bunduki.


Alidai kuwa baadhi ya vijana hao walikuwa na mafunzo ya kujihami na walifanya vitendo vya kihalifu katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

“Baada ya kubaini mtandao mzima, nilirudi kwa mkuu wangu wa kazi nikamuomba aniongezee nguvu niweze kuanza kutekeleza jukumu langu mara moja kutokana na aina ya kazi kwa sababu niligundua nilikuwa nachunguza watu hatari,” alidai shahidi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad