Shahidi Anadai Kesi ya Kina Mbowe ni ‘Mchongo’




Dar es Salaam. Shahidi wa pili wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, Lembrus Mchome ameibua tuhuma mahakamani akidai mawakili wa Serikali, mashahidi na majaji wa kesi hiyo kuwa ni michongo.

Shahidi huyo alitoa tuhuma hizo wakati akihojiwa na kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, muda mfupi baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi la upande wa mashtaka na kukubali kupokea nyaraka za shahidi huyo kuwa sehemu ya ushahidi wake.

Alipoulizwa na wakili Kidando kama ni kweli amekuwa aliandika maneno hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, alikubali na alipoulizwa maana yake akafafanua kuwa anavyoona mwenendo wa kesi hiyo mashahidi ni wa kutunga.

Na kuhusu maana ya majaji michongo alidai kuwa ni kwa sababu wamekuwa wakitoa uamuzi usio wa haki.


Wakati akitoa tuhuma hizo shahidi huyo aliwafanya wasikilizaji wa kesi hiyo kuangua vicheko huku Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo naye akishindwa kujizuia na kutabasamu huku akiendelea kurekodi ushahidi wake huo.

Mbowe na wenzake watatu waliowahi kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha makomandoo, Ngerengere, Morogoro, Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya wanakabiliwa na kesi ya kupanga kutekeleza na kufadhili vitendo vya kigaidi nchini.

Leo mawakili wa Serikali wanaendelea kumhoji shahidi huyo wa pili wa upande wa utetezi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad