MAWAKILI wa utetezi, katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, wamewasilisha ombi mahakamani la kukamatwa kwa shahidi wa 10 wa Jamhuri, Francis Mroso, wakidai kwamba alitoa rushwa ya Sh. milioni 90.
Akiwasilisha mahakamani ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Wakili wa Utetezi, Fridolin Bwemelo, alidai Sheria ya Kupambana na Rushwa kifungu cha 15(1B), inaeleza wazi hatua za kuchukuliwa kwa mtu atakayetoa na kupokea rushwa na hakuna kifungu kinachoeleza kuna rushwa ya kulazimishwa.
Alidai kwa mujibu wa kifungu hicho, hakuna sehemu imezungumzia suala la kutoa rushwa kwa kulazimishwa kwa kuwa mtoaji na mpokeaji wa rushwa watakuwa wametenda kosa.
“Mheshimiwa Hakimu, tunajiuliza ni kwa nini mtu aliyetoa rushwa na kukiri mbele ya mahakama hii bado yuko huru wakati waliopokea rushwa wameshtakiwa na wako ndani. Maombi yetu ili kuondoa utata kwenye jamii inayotuzunguka, tunaomba shahidi huyu akamatwe,” alidai Wakili Bwemelo.
Wakili huyo alidai kwamba mahakama imejiridhisha kupitia kwa shahidi ambaye yuko chini ya kiapo na kukiri kwamba alitoa rushwa ya Sh. milioni 90 na kwamba kesi hiyo ilipaswa kusikilizwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na si mawakili wa Jamhuri kama ilivyofanyika katika shtaka hilo.
Baada ya hoja hizo, mawakili wa serikali, Felix Kwetukia Tersila Gervas, walidai kwamba kwa kuwa wametuhumiwa kwamba hawakutakiwa kusikiliza kesi hiyo, watawasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ili kutoa ufafanuzi kwa nini walipewa ridhaa ya kusimamia kesi hiyo badala ya TAKUKURU.
“Tunaomba wiki mbili tuwasiliane na DPP, aliyetutuma kufanya kazi hii kwa sababu hata sisi tumetuhumiwa pia,” alidai Gervas.
Baada ya ombi hilo, hakimu aliahirisha shauri hilo hadi leo atakapotoa uamuzi mdogo endapo ombi la kukamatwa kwa shahidi huyo kama lina mashiko.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imetupilia mbali pingamizi la mawakili wa Jamuhuri wakitaka maelezo ya Mroso aliyoandika kituo cha polisi yasipokelewe mahakamani kama kielelezo cha ushahidi kwa kuwa utaratibu wa kisheria haukufuatwa.
Pingamizi hilo, liliwasilishwa mahakamani na Kwetukia na Gervas, mbele ya Hakimu Kisinda kwamba Mroso ambaye ni mfanyabiashara katika Jiji la Arusha, alikamilisha kutoa ushahidi wake mahakamani huko.
Akitoa uamuzi mdogo jana, Hakimu Kisinda, alitupa ombi la upande la mashtaka kwa kuwa haliendani na matakwa ya kifungu cha sheria ya ushahidi.
"Mahakama kwa kuzingatia kifungu cha 154 cha sheria ushahidi imeona pingamizi lililowekwa na upande wa mashtaka haliendani na matakwa ya kifungu hicho hivyo mahakama inapokea nyaraka hii kama kielelezo cha ushahidi,"alisema Hakimu Kisinda.
Awali Wakili Fridolin Bwemelo, aliwasilisha ombi la maelezo aliyoandika shahidi kituo cha polisi na nyaraka kupokewa kama kielelezo cha ushahidi mahakamani.
Bwemelo, alidai kwamba maelezo yaliyoandikwa na shahidi huyo yanatofautiana na ushahidi wake alioutoa mahakamani.
"Sheria imeelekeza wazi maelezo yaliyoandikwa na shahidi kituo cha polisi yanapotofautiana tunaruhusiwa kuutikisa ushahidi wake," alidai shahidi huyo.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Kwetukia alidai kwamba wanapinga kupokewa kwa nyaraka hiyo kwa kuwa utaratibu wa kuitoa haukufuata sheria.