MFANYABIASHARA Francis Mroso, amedai Mahakamani kwamba alifurahishwa na kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kumsimamisha kazi na kumtumbua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
Mroso, ambaye ni shahidi wa 10 wa Jamhuri katika kesi ya rushwa na uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya na wenzake sita, alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sylvester Nyegu, Enock Togolani, Watson Mwahomange, John Odemba, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Fridolin Bwemelo, Mrosso ambaye ni shahidi wa 10 katika kesi hiyo, alidai kwamba kitendo cha Rais Samia kumsimamisha kazi Sabaya kwa ajili ya kupisha uchunguzi kilimfurahisha sana.
Alidai kwamba tukio la Sabaya na wasaidizi wake kulazimisha kupatiwa Sh. milioni 90 lilifanyika Januari 22, mwaka huu.
“Siku ya tano ya kutoa fedha hizo, nilikwenda kutoa taarifa kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kennani Kihongosi (kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM- UVCCM) na alishangazwa na tukio hilo na kuahidi kulifikisha ngazi za juu,” alidai Mrosso.
Pia alidai kuwa alitoa taarifa kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salumu Hamduni, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alidai kuwa Hamduni naye aliahidi kulishughulikia suala hilo na alimwagiza Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO), kuchukua maelezo ya tukio hilo na kulifanyia uchunguzi.
Wakili Bwemelo alimuuliza shahidi kwa nini alienda kwa viongozi hao badala ya kwenda Kituo Kikuu cha Polisi na kujibu kwamba Sabaya alikuwa Mkuu wa Wilaya na ni mteule wa Rais, hivyo alikwenda kwa viongozi wa juu zaidi ili walishughulikie tatizo lake la kuchukuliwa kwa nguvu.
Mrosso alidai kuwa alipokuwa Benki ya CRDB Tawi la kwa Mrombo, Arusha, alikuwa chini ya ulinzi na vijana wa Sabaya ambao walijitambulisha kuwa ni maofisa usalama wa taifa na wengine maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo hakutakiwa kupiga simu wala kuongea na mtu yeyote.
Wakili Bwemelo alimwuliza Mrosso kama anamfahamu Cathbert Swai, mfanyabiashara maarufu wa mjini Moshi na kukaa naye kikao chochote, na kudai kuwa hamjui wala hajawahi kukaa naye sehemu yoyote kuzungumzia kitu chochote.
Pia alidai kuwa Kihongosi na Hamduni, hawajui zaidi ya kuwaona na kuwasikia katika shughuli zao za kila siku za kiserikali.
Alidai kwamba alikabidhi Sh. milioni 90 kwa vijana wa Sabaya, wakiwa katika eneo la Shule ya Msingi Sombetini, jijini Arusha, baada ya kuzitoa fedha benki na kuwekwa katika boksi.
Mrosso alidai baada ya kutoka benki aliongozana na vijana hao, hadi katika shule hiyo na aliamuriwa kupunguza mwendo wa gari lake na aliposhuka, kulikuwapo na gari lingine lililokuwa likiwafuata nyuma.
Katika kesi hiyo, shtaka la kwanza ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kifungu cha 57(1) na 60(2) na linawakabili washtakiwa wote.
Ilidaiwa Mahakamani huko, kwamba kwa pamoja washtakiwa hao, Januari 22, mwaka huu, katika maeneo tofauti jijini Arusha, akiwa mtumishi wa serikali kwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, walifanya vitendo vya uhalifu kwa kujipatia Sh. milioni 90 kwa manufaa yao.
Shtaka la pili ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa na linamkabili Sabaya kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kifungu cha 15(1B,2) Sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Ilidaiwa kwamba Januari 22, mwaka huu, eneo la kwa Murombo jijini Arusha, Sabaya alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Mroso, kumpatia Sh. milioni 90 kwa kumshinikiza ili asitoe taarifa za jinai za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.
Shtaka la tatu ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa, linalomkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kifungu cha 15(1B,2) sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Katika shtaka hilo, inadaiwa kwamba Januari 22, Sabaya akiwa katika eneo la Kwa Mrombo, alijihusisha na rushwa kwa kujipatia Sh. milioni 90 kutoka kwa Mroso ili asitoe taarifa za jinai za madai ya ukwepaji kodi.
Shtaka la nne ni la matumizi mabaya ya madaraka, inadaiwa kuwa Januari 22, Sabaya akiwa katika eneo la kwa Mrombo, alitumia vibaya nafasi yake ya Mkuu wa Wilaya ya Hai kwa kumtisha Mrosso kumfungulia mashtaka ya kukwepa kodi kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 15(9) cha Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa dhumuni la kujipatia fedha.
Shtaka la tano ni la utakatishaji wa fedha na linawakabili washtakiwa wote saba kinyume cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Sura ya 423 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Inadaiwa Februari 22 mwaka huu, Ole Sabaya kwa kushirikiana na wenzake, wakiwa katika eneo la kwa Mrombo, walijipatia Sh. milioni 90 wakitambua kwamba kufanya hivyo lilikuwa zao la vitendo vya rushwa.