Shemeji akamatwa mauaji ya mchungaji wa KKKT
JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia, Naftali Lulandala (40) mkazi wa kijiji cha Uhambingeto akituhumiwa kuhusika na mauaji ya Mchungaji Elizabeth Amosi (pichani) wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa.
Kwa mujibu wa Polisi mtuhumiwa huyo ni shemeji wa marehemu (mume wa mdogo wake) ambaye awali alikana kumfahamu mchungaji huyo ambaye alikuwa ndiye mwenyeji wake ingawa alitoa taarifa yha mauaji hayo.
Mwili wa Mchungaji Amosi ulipatikana Desemba 15, mwaka huu katika pori la Netomnachungu katika kijiji cha Kipaduka, Kata ya Uhambingeto tarafa ya Mazombe, wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alisema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na majeraha makubwa katika mkono wa kulia, jicho la kushoto na sehemu mbalimbali za mwili.
“Baada ya kufikishwa kituo cha Polisi Ilula na kupelekwa katika hospitali ya Ilula kwa ajili ya utambuzi, mwili huo haukuweza kutambuliwa kwa siku tatu mfululizo, Desemba 15 hadi 17 ulipozikwa,” alisema.
Alifafanua kwamba baada ya zoezi la kuutambua mwili huo kukwama, Ijumaa iliyopita serikali ya kijiji cha Ilula iliamua kuchukua jukumu la kuuzika.
Hata hivyo mume wa marehemu alipopata taarifa alifukua mwili wa mkewe na kuuzika upya kwa heshima ya familia katika kijiji chake cha Ilambilole, wilayani Kilolo, Jumamosi iliyopita.
“Mume wa marehemu alipata taarifa ya kifo cha mkewe kupitia picha na taarifa ya mauaji hayo zilizosambazwa na jeshi la Polisi katika mitandao mbalimbali ya kijamii,” alisema.
Akizungumzia uchunguzi wa awali wa mauaji hayo, Kamanda Bukumbi alisema Mchungaji huyo alikuwa akijihusisha na shughuli za kilimo na biashara ya alizeti kupitia mashamba ya kukodi katika kijiji cha Uhambingeto.
Kabla ya tukio hilo la mauaji, alisema Mchungaji huyo alikwenda katika kijiji hicho cha Uhambingeto akiwa na fedha mfukoni zaidi ya Sh milioni mbili kwa ajili ya shughuli yake hiyo ya kilimo na biashara.
Akiwa kijijini hapo Kamanda Bukumbi alisema uchunguzi wao unaonesha kwamba Mchungaji huyo kwa muda wote alikuwa na mwenyeji wake, Naftali Lulandala ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji hayo.
“Mtuhumiwa huyu ndiye aliyetoa taarifa ya mauaji hayo Polisi. Na katika taarifa yake Polisi alisema hamtambui marehemu huyo,”alisema.
Hata hivyo Kamanda Bukumbi alisema uchunguzi wao umebaini kwamba mtuhumiwa huyo (Lulandala) aliingia tamaa ya fedha, akapora na hatimaye kumuua Mchungaji huyo.
Mchungaji huyo ameacha mume na watoto watatu.