KLABU ya Simba imesema kuwa itakaa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), pamoja na Bodi ya Ligi ili kumaliza tofauti zilizojitokeza hivi karibu, ikiwamo kuzuiwa kuingia uwanjani kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez kwenye mechi dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita.
Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', amesema wameiandikia barua TFF na Bodi ya Ligi kuwasilisha malalamiko yao na kwa bahati nzuri wamekubali kukaa kuzungumza ili kuondoa kero na tatizo hilo ili lisijirudie tena.
"Sasa tunakwenda kutafuta suluhu, wamekubali kukaa na kuzungumza, hivyo nawasihi wanachama na mashabiki wa Simba watulie, litafikia muafaka na baada ya vikao vyetu tutatoa ufafanuzi ulionyooka, kwa sasa Wanasimba wajue kuwa viongozi wao wanalishughulikia suala hilo," alisema.
Alisema hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Barbara kuzuiwa, kwani hata yeye, na Mshauri wa Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Crescentius Magori walikumbana na kadhia hiyo.
Kuhusu ujenzi wa uwanja, Mwenyekiti huyo alisema watakaa kikao na hivi karibuni watatoa utaratibu wa wanachama kuchangia.
Kuzuiwa kwa Barbara ndiko kulikoibua hisia za mashabiki wa Simba kutaka kuchangia ili kuondokana na kadhia hiyo.