Simba imeshinda mabao 4-1 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Bao la kwanza la Simba limefungwa dakika 11 na mlinzi wa pembeni Mohamed Hussein wakati la pili likifungwa na mlinzi Onyango kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyopigwa na kiungo Larry Bwalya.
Bao la KMC limefungwa mchezaji Abdul Hassan kwa shuti Kali la chini lililogonga mwamba wa pembeni na kujaa wavuni ,mlinda mlango Aishi Manula akibaki anashangaa.
KMC ambao awali walikuwa kama wamepigwa butwaa ,walianza kuchangamka na kama wakiendelea kucheza kama walivyocheza dakika 15 mwisho za kipindi Cha kwanza, wataiweka Simba katika wakati mgumu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mashambulizi yaliyosababisha mabao mawili ya mapema yakifungwa na Kibu Denis dakika ya 47 na 57.
Bao la Kibu la dakika 57 liliibua shangwe baada ya kupiga shuti kali nje ya boksi na kumshinda mlinga mlango Faruk Shikhalo na kuzama wavuni.
Mbali na yaliyoendelea uwanjani jambo lilizoua gumzo ni mabadiliko ya Simba ambapo alionekana mlinzi Pascal Wawa kusubiri kuingia ila kocha mkuu Pablo alimzuia kwa kumsukuma akimrudisha nyuma.
Wawa alirudi benchi kisha aliitwa tena na kiungo Abdulswamad Kassim ila hakuingia na kutembea kurudi benchi. Viongozi wa Simba hawakuwa tayari kuzungumzia sakata hilo hadi wanaondoka uwanjani hapo.