Kama inavyotafsiriwa katika lugha, mila ni mambo yanayofanywa na jamii fulani ambayo yanalingana na asili, mazingira na nyendo za jamii hiyo.
Wachaga wana mila ambazo ni mambo wanayofanya kulingana na asili na mazingira yao. Na pia wana mambo wanayotenda kila siku ambayo kwao ni ya kawaida kabisa kiasi kwamba hawaulizi yalianza lini na kwa nini wao wanatenda hivyo.
Mila na desturi hizo hujumuisha masuala kama ndoa, mikutano, mavazi, vyakula, vinywaji wanavyokunywa na vyakula wanavyokula, lugha wanayoongea na heshima kwa koo na familia zao.
Safari za mwisho wa mwaka
Moja ya desturi zinazoheshimika kwa Wachaga wengi ni kutenga maeneo maalumu kwa shughuli za kimila kama vile kuchinja au kukutana kwa shughuli nyingine mbalimbali za ukoo.
Mara nyingi kukutana huko kunafanyika mara moja kwa mwaka. Na kipindi muhimu zaidi ni kile cha majira ya sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.
Kwa kawaida kila ukoo unakuwa na mwenyekiti wake ambaye kazi yake kubwa inakuwa ni kuita vikao, kusimamia na kukumbusha maadili na desturi za ukoo, kufundisha vijana maadili mema kama vile kutii wazazi, kukemea tabia chafu zisizoendana na maadili ya ukoo, kusimamia ndoa kwa vijana kwa kuzingatia misingi ya mila na desturi.
Katika vikao kama hivi ni kawaida kwa wanaukoo kuchinja ng’ombe au mbuzi, na mara nyingi hii hufanyika mwisho wa mwaka, na ndiyo sababu kubwa inayowafanya Wachaga wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na duniani kwa jumla, kurejea Uchagani wakati wa majira hayo ya mwaka. Kutokana na kitendo hicho cha kwenda kwa wingi Uchagani, baadhi ya watu wamekuwa wakiwafanyia utani kuwa huwa wanakwenda “kuhesabiwa”.
Katika kuhesabiwa huko, kila ukoo unakuwa na kikao rasmi kinachofanyika Desemba ya kila mwaka na kuwakusanya wanaukoo wengi kama si wote.
Hapo ndipo ndugu wanaotoka sehemu mbalimbali hukutana na kukumbushana mambo mbalimbali.
Mambo gani hufanyika wanaporudi?
Amani Ngowi ambaye kwa zaidi ya miaka 20, amekuwa akirudi nyumbani kila mwisho wa mwaka, anasema kipindi hicho hukitumia kufanya vikao vya ukoo, kufanya tathimini ya utekelezaji wa mipango ya mwaka unaoisha, kujadili matatizo na changamoto zilizojitokeza pamoja na kupanga mikakati ya mwaka unaokuja.
“Kikubwa ni kukutana kama familia na kuweka mikakati. Kwa mfano, katika familia yetu, sisi tunakutana kila Disemba 26, ambapo huwa tunazungumza mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika ukoo wetu,”anasema.
Anaongeza: “Kama kuna mtu ana tatizo na mwenzake, hiki ndicho kipindi tunasuluhishana ili kila mmoja amaliza vizuri kwa furaha na amani, lakini pia kila mmoja hutoa ratiba yake ya mwaka mzima unaokuja.
Kama ni kuoa, kuolewa, kujenga au chochote ambacho kinatarajiwa kufanyika mwaka huo ujao, kinawekewa ratiba na mikakati inapangwa.’’
Aidha, anasema kipindi hicho hutumika kutambulisha watoto wapya ambao hawafahamiki nyumbani.
“Lakini pia kama kuna mtoto ambaye amezaliwa nje ya ndoa, ni kipindi chake cha kutambulishwa nyumbani ili afahamike. Sisi huwa hatuachi damu yetu nje na ndio maana kipindi hiki hutambulishwa, ”anaeleza.
Anasema pamoja na kukutana kama familia, ni kipindi cha makanisa kuweka mipango ya maendeleo ambapo wao pia hukutana kwenye makanisa ya nyumbani walikozaliwa na kutoa michango ya maendeleo.
Akizungumzia utaratibu wa watu kunywa pombe sana na kuchoma mbuzi (ndafu) wanaporudi, Amani anasema ni sehemu ya furaha na kwamba ili mtu asherekee ni lazima ale na kunywa.
“Kula na kunywa ni sehemu ya furaha, sasa tunapokutana ndugu jamaa na marafiki ambao hatujaonana kwa mwaka mzima, ni lazima tufurahie kwa kula na kunywa, na huko ndiko kusherehekea kwenyewe, ” anaeleza.
Namna wanavyojiandaa mwaka mzima
Amani anaeleza kuwa, ili kufanikisha mipango ya vikao vya familia na siku kuu ya Krismmasi, watu hujiandaa kwa mwaka mzima, na hayo hufanyika kulingana na kipato cha mtu na uwezo wa ukoo husika. “Sisi kwenye ukoo wetu, kila mmoja anachangia Sh100,000 ambapo huwa tunanunua ng’ombe, vitu mbalimbali vya kupika na vinywaji, lakini zipo koo ambazo kutokana na uwezo wa kifedha, mtu mmoja anaweza kusema mwaka huu mimi nitagharimia kila kitu ukoo ufurahi,”anasema.
Anasema kiwango cha chini ambacho mtu anapaswa kuwa nacho ili kwenda kusherehekea sikukuu ya Krismasi ni Sh 500,000, kwa kuwa Desemba vitu vingi hupanda bei kuanzia kwenye gharama za usafiri.
“Kwa wale watu wa familia wasio na nauli ya kufika nyumbani au mchango uliopangwa na ukoo kuchangia kwa ajili vikao na sherehe ya pamoja, ndugu hulazimika kumchangia, lengo likiwa ni kuhakikisha wanakutana wote,”anasema.
Usikose mwendelezo wa simulizi hizi. Kesho tutaangazia umuhimu wa jani la sale kwa Wachaga na sababu ya jamii hiyo kuelezwa kuwa inapenda sana fedha hasa kupitia biashara.