“Sasa niko ‘single’ naenjoy, mwenzenu niko ‘single’ naenjoy, bora niko single naenjoy. Nikitaka kwenda kidimbwi, naenda naparty mpaka asubuhi halafu siulizwi.”
Hicho ni kibwagizo cha wimbo unaofanya vizuri kwa sasa kutoka kwa msanii Lavalava akieleza furaha yake ya kuishi bila mwenza.
Mbali na kibwagizo hicho, msanii Saraphina kwenye wimbo alioshirikishwa na The Baddest ameimba, “Oooh tuacheni utani, ‘single’ ni amani, hata nichelewe kurudi... na tukiwa na party popote nakwenda, kutoana roho kisa penzi haifai mwenzenu niko ‘single’ jamani napenda.”
Nyimbo zote mbili zinafanya vizuri kwa sasa kwenye vituo vya redio, runinga na chati mbalimbali za muziki kwa kuwa zinabeba ujumbe unaoelezea hali halisi inayoendelea kwenye jamii kwa sasa.
Kuna watu ambao wamekata tamaa ya kuwa na wenza au kupitia maumivu mbalimbali yanayowafanya waamini kuishi bila kuwa kwenye uhusiano ndiyo kitu salama zaidi kwao.
Licha ya kuwa suala hili liko kwa pande zote mbili, wanawake ndio wanaoonekana kuwa wafuasi wakubwa wa mawazo hayo, hali inayotishia kwamba, upo uwezekano idadi ya wanawake walio ‘single’ (wasio na wenza) ikaendelea kuongezeka siku hadi siku.
Mshauri wa Uhusiano, Deogratius Sukambi anasema endapo suala hilo halitaangaliwa kwa kina na jamii kuamua kuchukua hatua, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Sukambi anakiri kuwa wanaume wana mchango katika kutengeneza hali hiyo inayowafanya sasa wanawake wajione kuwa wanaweza kuishi bila kuwa kwenye uhusiano.
“Hatua zisipochukuliwa mapema kwa kuwajengea uwezo wanaume kwa kuwajibika na kuwafanya pia wanawake kuwaelewa wanaume, tatizo hili linaweza kuwa kubwa zaidi,” anasema Sukambi.
Mshauri huyo anasema kuna mambo yanayochochea wanawake kuamua kuishi bila kuwa na wenza, kubwa ikiwa ni uwezo wa wanawake kujimudu kiuchumi.
Anasema kadiri harakati za kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi zinavyoendelea zinawafanya wanaume wasionekane kuwa na umuhimu.
“Kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakiwategemea wanaume kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi ili kuendesha maisha yao. Jinsi mwanamke anavyoongeza uwezo wake kiuchumi inampunguzia ulazima wa yeye kuwa kwenye uhusiano na kumbana, mfano ndoa au familia,” anasema Sukambi.
Jambo lingine anasema ni hisia za wanawake kuona wana uwezo wa kufanya mambo ambayo yangeweza kufanywa na wanaume kwenye maisha yao, ikiwamo kujihakikishia usalama wa kimwili na hata kihisia.
Sababu nyingine ni maumivu na majeraha yanayotokana na uhusiano yamekuwa yakiwafanya wanawake kujiweka mbali na wanaume.
“Wapo wanaoona wenzao wakipitia mateso kwenye uhusiano na wapo walioanza kuyaona hayo tangu wakiwa wadogo, hii sasa inaweza kuwafanya waone uzito kuingia kwenye uhusiano,” anasema Sukambi.
“Matukio yanayoendelea kuripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu mateso na ukatili wanaopitia wanawake waliopo kwenye uhusiano inasababisha kuongezeka kwa wanawake wanaoamua kujiweka kando na uhusiano.”
Sababu nyingine inayosababisha kuongezeka kwa wanawake wasio na wenza ni kupoteza imani juu ya uwezo na uwajibikaji wa wanaume kwenye maisha ya wanawake.
Anasema wanaume siku hizi sio watu wa kujali, kupenda, kuthamini wala kutimiza wajibu wao kama wanaume au wazazi, hivyo hali hiyo inawafanya wanawake kupoteza imani.
“Wanawake wengi sasa wanaingia kwenye uhusiano kubahatisha. Ukisikiliza mijadala ya wanawake wengi wamepoteza imani kuhusu suala la wanaume kuwajibika au hata uwezo wa wanaume kihisia.
“Imefikia hatua mwanamke anaona hakuna sababu ya kujiingiza kwenye uhusiano ambao utamfanya bado aendelee kubeba majukumu ya kujihudumia sawa sawa na angekuwa bila mwenza,” ansema Sukambi.
Sababu nyingine anasema ni mtindo wa maisha ambayo imekuwa kama ‘fashion’ kwa wanawake kuamua kujiweka mbali na uhusiano na hata akijihusisha na mtu basi ni kwa ajili ya starehe sio kujizatiti.
“Sasa hivi kuna ‘fashion’ ya wanawake single, kundi la mabinti linaloibuka kwa sasa na kuonekana ni mfumo wa maisha na hawa ni wengi kuliko wanaosukumwa na hizo sababu nyingine,” anasema.
Wanawake wanasemaje?
Jane Ngowi (26) mkazi wa Dar es Salaam, anasema “kuna wakati unaona bora uwe mwenyewe kuepusha usumbufu. Unajua unaweza kuwa na mtu kwenye uhusiano akataka akufanye kama mtumwa, kama una moyo mdogo ule usumbufu unaweza kukufanya kuamua kuishi mwenyewe kisela.”
Akizungumzia sababu ya wanawake kuwa single, Asha Mkwanga (38) anasema mapenzi si kila kitu kwenye maisha, unaweza kuamua kuwa ‘single’ ili ujikite kwenye mambo yako mengine ya muhimu.
“Uhusiano unahitaji muda na kujitoa, sasa kama una vitu vingine vya muhimu vya kufanya inaweza kuwa vigumu kutimiza wajibu wako kwenye uhusiano na ndiyo usaliti utaanza, sasa bora uwe ‘single’ uenjoy,” anasema.
Kauli ya Asha inashabihiana na Gift Mlyego (30) ambaye anasema wanaume siku hizi wamekuwa pasua kichwa, wanasahau majukumu yao kiasi kwamba unaona hakuna sababu ya kuwa naye, ni bora uishi kwa kujitegemea mwenyewe.
“Uwe kwenye uhusiano ‘serious’ halafu hakuna tija yoyote unayopata ni ngumu kwa kweli.”