Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Kenya zimefanikiwa kuondoa vikwazo 46 vya biashara kati ya 64 vilivyokuwepo kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni utekelezaji wa makubalino yaliyofikiwa na viongozi wa nchi hizo mbili Mei, 2021.
Mbali na kuondoa vikwazo, pia wamewaagiza mawaziri wa biashara wa nchi hizo mbili kuendelea kukutana kuangalia vikwazo vilivyobaki na namna ya kuviondosha.
Ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 10, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na vyombo vya habari baada ya kusainiwa kwa mikataba ya mashirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afya.
Samia amesema katika utatuzi wa vikwazo hivyo, alimuomba Rais Uhuru Kenyatta watumie majina yao katika kutafuta suluhisho ya na vikwazo 64.
Amesema kupitia jina la Uhuru walisema sasa ni uhuru wa kufanya biashara Kenya na Tanzania na kupitia jina lake la Suluhu basi watafute suluhu ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
“Mwenzangu alinikubalia tukatumia majina, tumeondoa vikwazo 46 kati ya 64. Faida yake kuna ukuaji wa biashara, tumetoka Sh885 bilioni sasa ni Sh1.1 trilioni, hivyo kuna ukuaji mzuri wa biashara,” amesema Samia.
Katika upande wa uagizaji wa biashara amesema Kenya iliagiza bidhaa ndani ya Tanzania mara tatu zaidi ukilinganisha na mwaka uliopita huku Tanzania ikiuza bidhaa kwenda Kenya kwa kiwango tajwa awali.
Amesema pamoja na jitihada hizo, wamebaini bado kuna changamoto hivyo wamewataka Mawaziri wa biashara wa nchi hizo mbili kuendelea kukutana ili kuangalia zilizobaki ni zipi na namna ya kuodnoshwa.
“Kama ni kubadilisha sharia au sera twende huko tuondoe vikwazo ili biashara iweze kukua,” amesema Samia.
Amesema Tanzania na Kenya ni watani wa jadi na wakati mwingine wamekuwa wakitaniana hadi kutishiana lakini nchi hizo hazithubutu kupigana hata siku moja.
“Tunaudhiana, tunavimbiana kisha tunaambiana bwana hebu njoo tukae kwa pamoja, kwani shida nini anasema uliniambia hivi, hilo tu liishe bwana tunaendelea, hiyo ndiyo Kenya na Tanzania,”
Amesema pia Kiswahili kimekuwa kiunganishi kikuu huku akibainisha kuwa mazungumzo yote kabla ya kusainiwa kwa mikataba yamefanyika kwa lugha ya Kiswahili kizuri.
Amesema kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, nchi hizo zimefanya mazungumzo mara mbili ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni kati yake na Rais Uhuru na yale ya pili yakihusisha mawaziri.
Kati ya mengi waliyokubaliana kwanza walipitia kuangalia hali zao za uchumi ambazo zote zinaridhisha na kisiasa nchi zote ziko vizuri.
Katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kuna mambo mengi yanayo fungamanisha nchi hizo, ikiwemo mipaka ya ardhini katika mikoa mitatu ikiwemo Tanga, Mara.
“Na kuna mipaka ya bahari ya Hindi na Ziwa Victoria, pia kuna makabila sawa kama wajaruo, wamasai, wadigo, Watanzania na Wakenya ambao huwezi kutoa damu ya mdigo wa ukasema huyu ni wa Kenya au Tanzania.