SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefafanua taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez kuzuiwa kuingia kushuhudia timu yake ikicheza dhidi ya Yanga leo uwanja wa Mkapa.
Muda mfupi kabla mechi hiyo kuanza, kiongozi huyo alisambaza video na kuelezea kuwa amezuiwa kuingia uwanjani na ofisa wa Bodi ya Ligi akiwa na familia yake.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare tasa, ilieleza kuwa mtendaji huyo alizuiwa kuingia sehemu ya kukaa ya VVIP akiwa na watoto ambao hawaruhusiwi kuingia katika eneo hilo huku wakiwa na kadi za wau wengine walioalikwa kinyume na utaratibu unavyotakiwa.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Barbara yeye aliruhusiwa kuingia na alianza kutoa lugha isiyofaa kwa ofisa huyo huku akirekodi video na baadaye alitupa kadi hizo na kuondoka.
"TFF imesikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na baadhi ya viongozi wa Simba kwenye eneo la kuingilia Jukwaa la watu maalumu, pia viongozi wengine walifanya vurugu eneo la kuingili baada ya kutakakulazimisha mmoja wa viongozi kuingila bila kadi ya mwaliko," ilieleza taarifa hiyo ya Ndimbo