TMA yahadharisha mvua kubwa Dar, Pwani



 
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari kuwa mvua itaendelea kunyesha katika maeneo ya mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Kanda ya Ziwa.

Akizungumza na Nipashe jana, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Joyce Makwata, alisema kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Kagera na Geita) mvua zinazoendelea ziko nje ya msimu na zinatarajiwa kuendelea mpaka katikati ya mwezi ujao.

"Mikoa mingine hizi ni mvua za msimu ukiondoa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo mvua zake mara nyingi zinaisha Desemba, lakini hizi zitaenda mpaka Januari bado zitakuwa zinanyesha, hivyo tunawashauri wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya madhara yanayoweza kutokea," alisema Makwata.

Pia alisema wananchi waendelee kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na TMA ili kuchukua tahadhari.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omari Kumbilamoto, akizungumza na Nipashe jana, alisema mpaka sasa bado hakuna madhara makubwa yaliyotokana na mvua katika jiji hilo.


 
"Athari kubwa ambazo ziko mpaka sasa ni baadhi ya maeneo kuzungukwa na maji, lakini athari kubwa zaidi ya hapo hazijaripotiwa," alisema Kumbilamoto.

Pia alisema kwa sasa wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo na ushauri unaotolewa na mamlaka husika.

"Lakini hiki ndicho kipindi cha kuimarisha miundombinu. Kwa  mfano kwa sasa tunakazania na kusubiri kuona kama tutakamilisha ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi ili kukabiliana na athari za mvua kwenye Mto Msimbazi," alisema.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora, alisema mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo bado hazisababisha madhara, lakini zimeleta faida kwenye kilimo.

"Sisi tumepata mvua za wastani na bado zinaendelea. Zimefanya mazao kustawi kwa sababu tuliwashauri wananchi kulima mazao ya muda mfupi, hatujapata madhara makubwa tunashukuru Mungu," alisema.

Mvua zinazoendelea sasa kwenye baadhi ya mikoa nchini zilitabiriwa na TMA Septemba, mwaka huu, kwa mikoa inayopata mvua za msimu baadhi zilitarajiwa kumalizika mwezi huu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad