Tozo Miamala ya SIMU Huku Kicheko, Kule Kilio


 

Dar es Salaam. Ushindani wa utoaji huduma za kifedha kupitia simu za mkononi umefanya baadhi ya kampuni kupoteza wateja na nyingine kupata ongezeko.


Pia kupungua kwa wateja katika baadhi ya kampuni, hasa wale wa huduma za kifedha kumetajwa kuchangiwa na ongezeko la tozo za miamala ya simu zilizowekwa na Serikali.


Kwa mujibu wa Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo ya tatu ya mwaka 2021, inaonyesha kuwa mtandao wa Vodacom ulipoteza wateja 954,657 kati ya Juni hadi Septemba.


Ripoti hiyo ya Septemba iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha kuwa, Juni mwaka huu mtandao huo ulikuwa na watumiaji wa M-Pesa milioni 13.61 ambao walishuka hadi milioni 12.66.


Wakati Vodacom ikipoteza wateja, mitandao inayotoa huduma za Airtel money, Halo pesa, Tigo pesa, TTCL pesa na Ezy Pesa zilipata ongezeko la wateja.


Airtel ilipata ongezeko la wateja 169,876, Halotel (295,457), Tigo (227,763), TTCL (124,572), na Zantel (9,199).


ADVERTISEMENT

Hadi Septemba, wateja 127,783 walikacha kutumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi na kufanya idadi ya watumiaji kufikia milioni 33.154 kutoka milioni 33.282 waliokuwapo Juni mwaka huu.


Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia alisema yuko likizo.


Lakini Jumanne iliyopita Mworia alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema kupungua kwa wateja hao kunatokana na kuongezeka kwa ushindani kati ya watoa huduma za mawasiliano na tozo la miamala ya simu. Licha ya kupoteza watumiaji hao wa huduma za kifedha, Vodacom inabaki kuongoza katika umiliki wa soko la huduma za kifedha ikiwa na wateja 12,660,205 sawa na asilimia 38 ya soko. Tigo pesa inafuata kwa kumiliki asilimia 25 ya soko, Airtel asilimia 21, Halopesa asilimia 11, TTCL asilimia 3 na Ezypesa ikiwa na asilimia 2.




Tozo mpya


Tozo hizo zilianza kutumika baada ya bajeti kuu ya Serikali iliyopitishwa na Bunge Julai mwaka huu iliyopendekeza kuanza kutoza Sh10 hadi Sh10,000 katika kila miamala ya kutuma na kutoa fedha, kulingana na thamani ya muamala husika. Tozo hiyo ni tofauti na viwango vya sasa vilivyokuwepo hivyo itaongezeka juu yake.


Lakini baada vilio vingi vya wananchi juu ya tozo hizo, Serikali ilipunguza viwango vya tozo mpya ya Serikali kwa asilimia 30.


Mworia alisema ili kuhakikisha wanaendelea kubaki namba moja katika utoaji wa huduma za simu wataendelea kuwa wabunifu.


“Tutaendelea kuongeza ushirikiano na wadau wengine ili tuweze kutoa huduma nyingine badala ya kutuma na kutoa fedha pekee. Tumejipanga kuwaletea wateja wetu huduma za kibunifu zaidi,” alinukuliwa Mworia.


Meneja wa T-PESA, Lulu Mkude alisema mafaniko yaliyopatikana ndani ya kipindi hicho yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kampeni ya kuwajengea uelewa wananchi kuhusu matumizi ya T-Pesa. Kupitia kampeni hii, tulisogeza huduma zetu za kifedha katika maeneo ya vijijini, jambo lililofanya tuongeze wateja. “Pia kiwango cha makato wanachotumia kimekuwa kikiwavutia wateja wapya na wa zamani,” alinukuliwa Lulu na The Citizen.




Wachambua sababu


Akizungumzia suala hilo, Mtafiti Mwandamizi, Profesa Samuel Wangwe alisema watu wengi wanatumia mtandao zaidi ya mmoja, hivyo wanaangalia sehemu ambayo ina unafuu wa vifurushi.


Naye Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo alisema tozo ndiyo sababu kubwa inayofanya kupungua kwa watumiaji wa huduma hizo za kifedha. Alitolea mfano kuwa Sh200,000 ikiwa katika simu tozo ni Sh6,500 wakati katika ATM kutoa kiasi kama hicho cha fedha ni Sh 1,600 ambayo ni ndogo mara tatu ya kwenye simu.


“Watu walikuwa wanatumia simu kwa sababu inafikika na gharama nafuu, lakini inapokuwa gharama ziko juu inamfanya mtu kuona ni vyema kwenda ATM badala ya kutoa kwa simu,” alisema Dk Kinyondo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad