Saif al-Islam al-Gaddafi
KAMATI ya Bunge nchini Libya, imetangaza leo Jumatano tarehe 22 Desemba 2021, kwamba haitawezekana kuandaa uchaguzi wa rais uliosubiriwa kwa muda mrefu katika siku mbili zijazo kama ilivyopangwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza hilo ni pigo kubwa kwa juhudi za kimataifa za kuumaliza muongo mmoja wa machafuko katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta.
Hii ni taarifa ya kwanza rasmi kuwa uchaguzi huo hautofanyika Ijumaa, ijapokuwa hilo lilitarajiwa kutokea kutokana na kuongezeka kwa changamoto nyingi na wito wa kutaka uchaguzi huo uahirishwe.
Katika barua yake kwa Spika wa Bunge Aguila Saleh, Mwenyekiti wa Kamati wa Kamati ya Bunge iliyopewa jukumu la kusimamia na kufuatilia mchakato wa uchaguzi, Al-Hadi al-Sagheir, amesema wamegundua uchaguzi huo hauwezi kuandaliwa 24 Desemba 2021, kama ambavyo ulipangwa.
Hakufafanua kama tarehe nyingine imepangwa, au kama uchaguzi huo umefutwa kabisa.
Taarifa ya Bunge ya kughairisha uchaguzi huo, imekuja siku moja baada ya Tume ya uchaguzi kuzivunja kamati za uchaguzi, na kutotaja orodha ya mwisho ya wagombea kama ilivyohitajika kufanyika kwa mujibu wa sheria.
Wananchi wa Libya, walitarajia kufanya uchaguzi wao wa kwanza ambao ungewapa nafasi ya kuchagua rais Ijumaa wiki hii.
Aidha, uchaguzi huo, ulitarajiwa kuhitimisha mpango wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa unaolenga kurejesha utulivu na kuiingiza madarakani serikali ya kidemokrasia, pamoja na kumaliza mzozo wa muongo mmoja.
Muda mfupi baada ya tangazo hilo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), ulitoa taarifa na kuonyesha wasiwasi wake juu ya hali ya usalama katika mji mkuu Tripoli.
Ulisema, “kuwapo kwa makundi ya kujihami, kunatishia kuwapo kwa mvutano na kusababisha uwezekano wa kuzuka upya kwa mapigano.” Umesisitiza kuwa “mizozo ya kisiasa inapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.”
Picha zilizochapishwa mitandaoni zimeonyesha vifaru na malori ya kijeshi katika wilaya ya Fornaj huku watu waliojihami kwa silaha wakishika doria katika baadhi ya barabara. Wakazi wamesema shule na vyuo vikuu mjini Tripoli vimefungwa kama tahadhari.
Wagombea 80 wamejitosa katika kinyang’anyiro cha urais, akiwamo mtoto wa rais wa zamani wa taifa hilo, Moamer Gadaffi, aitwaye Saif al-Islam al-Gaddafi.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Stephanie Williams licha ya kutotangaza rasmi kufutwa kwa uchaguzi huo, amekuwa akikutana na wagombea wa Urais wiki hii wakati 17 kati ya yao, wakisema kwa jinsi hali ilivyo, uchaguzi huo hauna budi ila kuahirishwa.
Jana Jumanne, mbabe wa kivita, Khalifa Haftar alikutana na wagombea wengine wawili wa urais – aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fathi Bashagha na naibu waziri mkuu wa zamani, Ahmed Maiteeq – mjini Benghazi.
Maiteeq aliwaambia waandishi wa habari, kwamba mkutano huo unatoa ishara ya matumaini kwa Walibya.
Alisema, “daima, Walibya wanaweza kuiongoza nchi katika hali ya utulivu. Libya ina uwezo wa kukabiliana na changamoto ili kuisaidia kusonga mbele.”
Hata hivyo, haikuwa bayana ni kipi hasa kilichowakutanisha watatu hao lakini mshauri wa Bashagha ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, sababu ya ziara yao mjini Benghazi ilikuwa ni kuondoa vikwazo na kuuonyesha ulimwengu kwamba wanaweza kuungana