Uongozi UDOM watetea PhD za mawaziri, wabunge



Dar es Salaam. Siku mbili baada ya shahada za uzamivu (PhD) za viongozi wa kisiasa hasa mawaziri na wabunge kuibua mjadala, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umezitetea na kueleza namna ya kuondoa shaka juu yake.

Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Faustine Bee amesema wenye shaka wanaweza kujiridhisha kwa kutembelea maktaba ya chuo hicho kuona machapisho ya wahitimu wenyewe.

Alisema suala la viongozi wakubwa kuhitimu shahada za uzamivu ni la muhusika mwenyewe anavyojipanga, kupangilia muda wake na majukumu aliyonayo.

“Ni suala la nidhamu ya muda, mtu kupangilia muda wake wa kazi na masomo kwa kuzingatia taratibu na maelekezo ya chuo na wasimamizi. Mimi sioni shida mtu kuhitimu kama anazingatia hayo,” alisema Profesa Bee


 
Profesa Bee alisema watu wengi wanaosoma shahada ya uzamili na uzamivu wakati wanafanya kazi na wana majukumu mengi, hivyo si sahihi kumhukumu mtu kisa ni mwanasiasa.

Profesa huyo alisema kama mwanafunzi anayesoma anayo nidhamu ya muda, licha ya majukumu yake, lazima atapata wasaa wa kukusanya taarifa.

“Hapa tuna walimu wengi wanasoma uzamivu na wanaendelea na kazi zao za kufundishia wakati nao wanasoma, hivyo suala sio nani, bali vigezo. Wote hao (mawaziri, wabunge) wamefuata utaratibu wa usimamizi na kuwasilisha mawasilisho ambayo waliyatetea mbele ya jopo la wanataaluma,” alisema Profesa Bee.


Alisema mtu kazi kama si ya kwake, angeshindwa kuitetea, lakini wote walitetea kazi zao vizuri na taarifa na machapisho yao yanapatikana katika chuo hicho na watu wanaweza kuyaona kwa kuwa ni ya umma.

Mjadala huo uliibuliwa juzi na mwanazuoni na mwanasiasa mkongwe, Profesa Mark Mwandosya alipoandika kupitia Twitter: “Nawapongeza wanasiasa mliotunukiwa shahada za uzamivu, udaktari wa falsafa. Nawafahamu mna uwezo mkubwa. Lakini inawezekana kweli ukawa mbunge na waziri, ukapata muda wa utafiti na kuandika tasnifu, hata ya uzamili ni kazi sana. Swali kwa vyuo vikuu, je, vigezo au viwango vimebadilika?” alihoji Profesa Mwandosya.

Mbali ya kuwahi kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwandosya pia aliwahi kuwa mbunge na waziri katika Serikali za tatu na nne.

Swali hilo limewaalika wanazuoni mbalimbali na mijadala kwenye mitandao ya kijamii, baadhi walimpinga na wengine wakimuunga mkono.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad