HUKU familia zilizopoteza wapendwa wao katika mkasa wa Mto Enziu katika Kaunti ya Kitui zikiendelea kuomboleza, utata umezuka kuhusu idadi kamili ya watu waliofariki katika tukio hilo la Jumamosi.
Shughuli ya kusaka miili ilisitishwa jana huku maafisa wa serikali wakisema idadi kamili ya waliofariki katika mkasa huo ni 32. Vile vile, manusura 16 waliokolewa kutoka kwa mabaki ya basi hilo lililokuwa likiwasafirisha wanakwaya kuenda harusini.
Hii inafikisha 48, idadi jumla ya watu waliokuwa ndani ya basi hilo lenye uwezo wa kubeba watu 51. Basi hilo ni mali ya shule moja ya kibinafsi iliyoko mjini Mwingi.Hata hivyo, manusura kadha walidai kuwa basi hilo lilikuwa limejaa kupita kiasi lilipokuwa likivuka Mto Enziu, huku abiria 15 wakiwa wamesimama.
Habari hii imeibua hofu kwamba huenda kuna watu wengine ambao bado hawajapatikana, japo idadi yao haijulikani.Kamanda wa Polisi katika kaunti ndogo ya Mwingi Mashariki Joseph Yakan alisema kwamba walikamilisha shughuli ya kusaka miili kwa sababu hakuna familia iliyojitokeza kudai kwamba bado hawajapata wapendwa wao.
“Shughuli ya uokoaji imesitishwa rasmi baada ya mtambo kufeli kupata miili zaidi baada ya kuchimba mchanga mtoni humo kwa saa kadha,” akasema kamanda huyo wa polisi.Hata hivyo, Bw Yakan alitoa wito kwa wakazi kupiga ripoti kwa polisi iwapo watapata maiti yoyote kando ya mto huo.
“Wananchi watujulishe ikiwa watapata miili yoyote baadaye ili tuje kuichukua na kuitambua,” akasema.Utata uliibuka kuhusu idadi kamili ya abiria waliokuwa katika basi hilo baada ya kubainika kuwa baadhi ya wasafiri waliokwama kando ya mto huo waliabiri basi hilo ili wavukishwe hadi ng’ambo ya pili.
Wasafiri
Baadhi yao walikuwa wakienda harusini katika mji wa Nuu ilhali wengine walikuwa wakielekea makwao kutoka mjini Garissa.Bw Simon Kea ambaye alinusurika katika mkasa huo, alisema basi hilo lilikuwa na abiria 40 lilipoanza safari mjini Mwingi Jumamosi asubuhi.
Bw Kae, ambaye ni muuguzi katika Hospitali ya Kimisheni ya Tei basi lilipoanza kuvuka, lilijaa abiria kiasi kuwa watu 15 walisimama.