Vyama vipya vya siasa 10 vyaomba usajili



Rais Samia Suluhu Hassan
IKIWA imebaki miaka minne kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 nchini Tanzania, zaidi ya vyama 10 vipya vimeomba usajili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezwa leo tarehe 15 Desemba, 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan wakati akifungua mkutano wa wadau kujadili demokrasia ya vyama vingi ulioandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia amesema maombi hayo ya vyama hivyo yapo mezani kwa msajili ambaye ndiye mwenye uamuzi wa kuwavipatia usajili vyama hivyo au lah!

Rais Samia amesema katika kukuza na kudumisha demokrasia ya vyama vingi vya siasa, sheria zilizotungwa na bunge zimewezesha vyama 19 kusajiliwa na kufanya kazi.


 
“Nimeambiwa vingine zaidi ya 10 vimeomba usajili na msajili anaendele na hatua za au ndio au sio,” amesema.

Itakumbukwa kuwa mapema Novemba mwaka huu, chama kipya kinachofahamika kwa jina la Umoja Part (UP) kilijitokeza hadhara kupitia kwa Mwenyekiti wake, Seif Maalim Seif kuomba usajili wa muda katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini.

Hata hivyo, hadi sasa haijafahamika, vyama hivyo vingine vya siasa vinaongozwa na watu gani ilihali kumekuwa na ming’ono kutoka kwa wadau wa siasa kwamba baadhi ya makada wa CCM wenye uelekeo wa kujiengua ndani ya chama hicho, wameanzisha chama kipya.


Pamoja na mambo mengine, akiendelea kuzungumza katika mkutano, Rais Samia amesema sheria mbalimbali nchini zimeruhusu uwepo wa taasisi za kiraia zinazotoa elimu ya uraia, kisiasa, kijamii na kiuchumi.

“Serikali imekuwa ikipokea na kuzifanyia kazi na hoja zinazotolewa na tathmini zinazofanywa na taasisi hizo na kuzifanyia kazi ipasavyo kwa lengo la kuleta ustawi wa demokrasia nchini.

“Nazipongeza taasisi hizo kwa maoni yao ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa chachu ya kuimarisha demokrasia yetu,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa duniani kuna taifa moja tu linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni taifa huru, lililojengwa katika misingi ya amani, upendo, mshikamano.

Amesema ni taifa linaloongozwa kwa misingi ya katiba na sheria zilizotungwa na Bunge sio kwa utashi wa mtu au utashi wa taifa lingine.

“Wenye hili taifa ni sisi tuko hapa, uendeshaji wa hili taifa utatokana na sisi tulio hapa. Pia ni muhimu kutambua kwamba demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini itakuwa na maana kama tukidumisha amani na utulivu na umoja wa taifa letu,” amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad