Na Philemon Muhanuzi
Ipo tofauti ya wazi kabisa kati ya ushabiki wa timu za Ulaya na huu wa kwetu. Wazungu wanauchukulia mpira ni sehemu ya ubinadamu kwanza, kabla ya kuwa na mawazo yoyote hasi juu ya mchezaji au wachezaji fulani.
Huwezi kuwakuta wamenuna kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho huku wakimtafuta wa kumzomea wakati mechi inaendelea.
Wanawapenda wachezaji wanaojituma muda wote wa mechi. Na penye wengi hapakosi wasanii kwa maana ya watunzi wa nyimbo za haraka haraka. Tunao pale Uwanja wa Taifa na wapo wengi katika viwanja vya ligi kuu za Ulaya hasa Uingereza.
Anaanzisha nyimbo shabiki mmoja na inadakwa upesi na wanaomzunguka. Mchezaji akisikia nyimbo inayochangia kumpandisha mzuka atajituma zaidi na zaidi.
Mohamed Salah akilisikia jukwaa zima linataja jina lake kwa pamoja hata kama hataonyesha kuguswa, ataendelea kufanya mazoezi magumu ili litajwe tena na tena.
Wapo wachezaji wengi wazalendo wanaochelewa kuonyesha kuwaelewa makocha wao kwa sababu tu ya namna mashabiki wetu wanavyoupokea uchezaji wao. Mchezaji atatoa pasi inayozaa goli, atawapunguza mabeki mara tano kwa juhudi binafsi lakini akikosa goli la wazi mara moja tu atalaumiwa na mashabiki watasahau juhudi zote alizoonyesha kuanzia dakika ya kwanza.
Simon Msuva ana roho ngumu sana kuweza kufika alipofika. Alipokelewa kwa matusi na mashambulizi ya kumkatisha tamaa, lakini alipambana mpaka mwisho.
Namuona Kibu Dennis akipitia katika kipindi cha kufanya makosa mengi kabla ya kujiamini kwake hakujaongezeka. Ni katika kipindi hiki anachopitia ndipo uwezo wake wa uvumilivu wa kichwani unapopimwa kama utaweza kumsaidia siku zijazo au la.
Mashabiki wa Liverpool walimuimba Mo Salah kama mfalme mpya wa Misri, ni maneno yanayompa mzuka kila anapoingia uwanjani.
Kwa sasa wanamuimba Mreno Diogo Jota, wanamjenga ili awafungie magoli kila anapokuwa uwanjani. Hii hulka ni tofauti kabisa na ile ya kupenda kumzomea mchezaji kijana ambayo ndio inayowatambulisha mashabiki wetu pale Uwanja wa Uhuru na ule wa Taifa.