Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba ameibua upya mchakato wa mabadiliko ya Katiba katika mkutano wa Baraza la vyama vya siasa na wadau wa demokrasia uliomalizika leo jijini Dodoma.
Katika mjadala uliokuwa ukiongozwa na Makamu mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandara, Jaji Warioba ameshauri pia suala la kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi na mkutano ya vyama vya siasa kufanyiwa kazi haraka.
“Kwanza ni mikutano ya vyama vya siasa. Rais ametoa mwelekeo, mimi nina hakika mkizungumza vizuri, hiyo tutamaliza.
“Pili ni Katiba; wananchi walishaamua, mchakato ukawapo, tukawa na rasimu, hakuna haja ya kusema turudi nyuma hatua zilizopita,” amesema Jaji Warioba.
Amefafanua kuwa mchakato wa Katiba unaongozwa na sheria na ipo, hivyo akashauri kuwa ifanyiwe marekebisho ili kuendana na wakati na mahitaji.
“Bado tunaweza kutafuta utaratibu wa ku-amend ile sheria ikatoka haraka na kuangalia, tunayo Katiba pendekezwa na kusahihisha mambo mengine, kisha tukaikamilisha,” amesema.
Kuhusu Tume huru ya uchaguzi, Jaji Warioba amekosoa uchaguzi mkuu wa mwaka jana akitaka sheria na kanuni za uchaguzi ziangaliwe upya.
“Kipindi hiki yametokea matatizo makubwa mno, kwa mara ya kwanza watu wengi wameenguliwa. Hawa Watanzania wamezoea uchaguzi tangu mwaka 1961, tangu 1958, yanakuja kutokea haya katika kipindi hiki, ni lazima kuna tatizo, ni lazima tujitazame, turekebishe.
“Mimi sijui kwa nini tunagombana juu ya hili. Kila baada ya uchaguzi ilikuwa ni kawaida yetu kuona udhaifu uko wapi kisha tunafanya mabadiliko,” amesema.