Polisi wilayani Kassanda nchini Uganda wanachunguza mauaji ya Emmanuel Deus, mtunza fedha wa Kampuni ya GEM James Gold Processing yanayodaiwa kutekelezwa na Watanzania watatu.
Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Monitor la Uganda, Deus aliripotiwa kupigwa hadi kufa na kundi la raia sita wa Tanzania Jumamosi iliyopita katika Halmashauri ya Mji wa Bukuya, Wilaya ya Kassanda.
Mwananchi jana lilimtafuta Mkurugenzi wa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Emmanuel Buhohela aliyesema bado hawajapata taarifa hiyo na kuahidi kuifuatilia.
Kwa mujibu wa polisi, Deus alikutana na kundi la Watanzania wanaojishughulisha na biashara ya dhahabu, wakinywa pombe huko Bukuya na waliingia katika ugomvi uliosababisha watuhumiwa hao kumpiga hadi kupoteza fahamu.
“Alikimbizwa katika Kliniki ya Bukuya na baadaye marafiki zake walimhamishia katika Hospitali ya Rufaa ya Mityana.
“Alitangazwa kuwa amefariki dunia alipofikishwa katika hospitali hiyo kutokana na kuvuja damu nyingi eneo la kichwani,” alisema msemaji wa Polisi, Fred Enanga katika taarifa yake ya jana kwa vyombo vya habari.
Enanga alisema watuhumiwa watatu ambao wote ni raia wa Tanzania ni Lubolo Erican, David Malingita na Peter Matunganjo aliosema wamewatia mbaroni.
“Vitendo kama hivi vya vurugu, mashambulizi na kupigana, vinatukumbusha hatari ambazo watu hukabiliana nazo wakati wa vurugu.
“Tunatumaini kukamatwa kwa washukiwa hao kutaleta ahueni kwa familia ya marehemu,” alisema msemaji huyo wa polisi.