Wazazi CCM ‘wapasuana’ Kisa Kauli Tofauti za viongozi na Makada wa Chama Hicho



Dodoma. Msuguano ndani ya chama tawala sasa ni dhahiri kutokana na kauli tofauti za viongozi na makada wa chama hicho kikongwe nchini.

Hivi karibuni kumekuwa na sintofahamu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hali iliyowalazimu wajumbe wake wa Kamati Kuu na makada wake watatu kujieleza kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Walioitwa kujieleza ni Mbunge wa Kuteuliwa Humphrey Polepole, Jerry Silaa (Ukonga) na Josephat Gwajima (Kawe).

Kama hiyo haitoshi, wiki iliyopita mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo alimshambulia Polepole akimtuhumu kukichafua chama.


Kutokana na mwendelezo huo wa matukio, jana iliibuka sintofahamu kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Wazazi lililosema kuna watu wasiofaa ndani ya chama hivyo kuwataka kuondoka. Vilevile zilitajwa njama za kuwabeba wagombea na tuhuma za kuuza shule ya jumuiya hiyo kinyemela.

View this post on Instagram
A post shared by Mwananchi (@mwananchi_official)

Katika mkutano huo uliofunguliwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemera Lubinga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, alizungumzia shule za jumuiya hiyo kuuzwa kwa bei ya kutupwa na waliouzawanatembea kifua mbele badala ya kuona aibu.


“Mkoa wa Mbeya ndio uliongoza kwa kuwa na shule nyingi za wazazi, lakini nashangaa hatuoni kitu, watu wameuza, fedha hazionekani, ramani na viwanja vimefichwa bado hawajali, hatuwezi kwenda namna hiyo ndugu zangu,” alisema Lubinga.

Kukithiri kwa madeni na kushindwa kujiendesha alisema kulikuwa kunaiua Jumuiya ya Wazazi, lakini chini ya mwenyekiti wake, Dk Edmund Mndolwa bado imesimama.

“Mimi nimekuwa mwenyekiti wa bodi ya shule ya wazazi, najua shule zilikuwa tajiri lakini kwa sasa zimeuzwa, hela hazionekani, walimu hawana mishahara na hatuoni aibu jamani. Ni vema kuwa waungwana tukatenda jema,” alisema Lubinga.

Kuhusu kupotea kwa viwanja na ramani, alisema anayefuatilia na kuuona ukweli anaonekana adui. Aliutaja pia Mgodi wa Dhahabu Geita kwamba uliuzwa kwa Sh50 milioni, lakini zilionyeshwa Sh20 milioni.


Kanali Lubinga aliwaagiza viongozi kuifuatilia Shule ya Hedaru ambayo alisema imeuzwa wakati vifaa vyote vimepotea na havijulikani viliko, magari yamegeuzwa daladala ila fedha hazionekani.

Bulembo atajwa

Wakati mkutano huo ukiendelea, alisimama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Mrida Marocha aliyemtaja Abdallah Bulembo kuwa yeye na kundi lake walishiriki kuiuza Sekondari ya Isango. Alisema walifanya hivyo saa mbili usiku kwa bei ya Sh70 milioni.

Marocha alisema shule hiyo alikabidhiwa Mwalimu Nyerere na wakoloni maalumu kwa ajili ya wasichana na alitumia nafasi yake kuwapa wazazi, lakini wachache waliiuza na kugawana.

“Shule ile ndiyo alisoma Gaudencia Kabaka (mwenyekiti wa UWT Taifa), Bulembo namtaja hata kama ana watu wake hapa wakamwambie, aliyeichukua ameanza kuipaka rangi,” alisema Marocha.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dk Edmund Mndolwa alikiri kuwa na taarifa za mgogoro wa Shule ya Isango, akisema kuna wakati alikaa hapo hadi usiku lakini mgogoro wake ni mkubwa.

Akijibu tuhuma hizo, Bulembo alisema “muulize huyo (Marocha) aliingia lini kwenye chama kama si mwaka wa tano huu, hajui chochote, nimehangaika na shule hiyo kwa miaka minne Mahakama Kuu nikitaka kuinasua kutoka kwa mfanyabiashara mmoja wa Musoma, mimi hata niliposhika nafasi ya mwenyekiti nilikuwa natokea Mara kwa hiyo nayajua mengi.”

Bulembo alisema Marocha hajui historia zaidi ya kuibukia kwenye uongozi na kutaka aseme ili asikike, huku akieleza kuwa yeye (Bulembo) ni mstaafu anayeweza kuwa na udhaifu lakini hauhusu uuzaji wa shule za jumuiya.

Kubeba wagombea

Kanali Lubinga pia aliuambia mkutano huo kuwa kuna taarifa za baadhi ya viongozi walioanza kuwabeba wagombea kwenye uchaguzi wa ndani utakaofanyika mwakani.

“Simu yangu ina whatsapp zenye ushahidi na katibu mkuu anafahamu yote. Chama kimelazimika kufanya mabadiliko ya viongozi kutokana na mwenendo usioridhisha na hakitasita kuchukua hatua,” alisema Lubinga.


Kanali huyo aliwakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa Jumuiya ya Wazazi ilikuwa inakaribia kufutwa lakini leo imeimarika na imepata wabunge.

Alisema CCM haina nia ya kuwafukuza wanachama wake, lakini inapobidi itawatimua, kwani hawawezi kuwa na watu wasiojua dunia inakwenda mbio na akataka wenye mtazamo huo wajiondoe.

“Kuna mtu alisema CCM si kitu kwake lakini tulipomfukuza akahoji ‘mnanifukuza mnataka nife kwa sababu sijui kitu nje ya chama hiki’ hata wanaume aliwajulia ndani ya chama, hivyo ukitoka utaona umuhimu wa chama,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad