Wakati Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akitinga kwa mara ya pili katika Stendi ya Magufuli jijini Dar es Salaam, Mwananchi limebaini kuwa abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali bado wanalanguliwa nauli ikiwa ni kinyume na maagizo ya Naibu waziri
Waitara juzi alifanya ziara ya kwanza ya kushtukiza na kubaini madudu ikiwamo watu kutozwa nauli kubwa kisha alitoa maagizo kwa viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kwa kushirikiana na askari wa usalama barabarani, kusimamia kwa kuhakikisha abiria wanakata tiketi kwa kiwango kinachotakiwa.
Pamoja na maagizo hayo, mambo yaliendelea kwenda mrama kwa jana. Kwa mfano, abiria waliokuwa wanasafiri kwenda Arusha walikuwa wanatozwa Sh 30, 000 wakati kiwango kinachotakiwa ni Sh22, 000 huku wanaoelekea Tanga wakilanguliwa 22,000 wakati kwa siku za kawaida wanalipishwa Sh 15000.
Huo ni mtindo mpya uliobuniwa na mawakala katika kipindi hiki cha skukuu za mwisho wa mwaka kujinufaisha
Wanakubaliana na wapiga debe na wanawauzia tiketi zote za basi husika na abiria anapokwenda ofisini kuhitaji tiketi, anaambiwa nafasi zimejaa, huku mteja huyo akielekezwa kwenda kuangalia kwenye mabasi hayo kama kuna uwezekano wa kupata nafasi.
Kwa kuwa ni mpango uliosukwa, abiria akifika kwenye basi husika, anakutana na wapiga debe wakiwa wameshika tiketi nyingi mkononi zilizokatwa kabisa na kuandikwa kiwango kilichoelekezwa na Latra, lakini wakiwa wanaziuza kwa bei ya juu. Mwananchi lilipomuuliza mmoja wa wakala ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake, alieleza kuwa mpango huo ulifanyika tangu siku sita zilizopita ambapo wapiga debe waliuziwa tiketi hizo ili wauze kwa bei ya juu kwa kutambua siku hizi za mwisho wa mwaka kunakuwa na tatizo la usafiri.
“Katika mpango huu wa kuuziwa wapiga debe tiketi, nao mawakala wananufaika kwa kugawana kiwango kinachopatikana hivyo inakuwa vigumu kwa Latra kufuatilia na kuwakamata kwani kwenye tiketi kunaandikwa kiwango kilekile kinachoelekezwa na mamlaka,”alisema wakala huyo.
Waitara atinga kwa mara ya pili
Waitara aliyetinga kwenye stendi hiyo saa 11: 30 alfajiri baada ya kuangalia hali halisi, alisema wahusika wameendelea kukaiidi maagizo aliyotoa, hivyo alipandisha kiwango cha faini hadi kufikia Sh 500, 000 kwa wale watakao bainika kuendeleza mtindo huo. “Tumekubaliana abiria alipe nauli halali, lakini kama amezidishiwa kanuni ya 42 inasema anaweza kupigwa adhabu Sh 200,000 hadi Sh300, 000 au kupelekwa mahakamani kwa kuwa nilikuja hapa juzi na nilitoa maelekezo. Kuanzia leo atakayefanya kosa hilo faini ni Sh 500,000 bila maelezo,” alisema Waitara
Katika maelezo yake, aliwataka wananchi kuonyesha ushirikiano kwa watendaji, ikiwa watazidishiwa nauli, basi wachukue namba za simu wapige kwa kutoa ushuhuda na wanaobainika kukiuka maagizo ya Serikali watachukuliwa hatua.