Wizara yatoa waraka shule kukiuka miongozo



 
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa waraka kwa shule zote nchini za msingi na sekondari kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo, badala ya ukiukwaji kwa madai ya kutafuta ubora na ufaulu wa wanafunzi.

Ni hatua inayojiri wiki chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, kupiga marufuku wanafunzi kusoma saa za ziada usiku na wakati wa likizo shuleni, akisema anaunga mkono taarifa za athari kwa wanafunzi iliyotolewa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

“Kutokana na kuongezeka kwa shule zinazokiuka taratibu, wizara inatoa maelekezo haya ili kusisitiza umuhimu wa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo iliyopo. Kalenda iliyowekwa katika utekelezaji wa mitaala izingatiwe kikamilifu sambamba na nyaraka zote za elimu, anatamka Kamishna wa Elimu, Dk. Lyabwene Mtahabwa.

Waraka wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia uliotolewa Jumatatu wiki hii na Kamishna wa Elimu, Dk. Mtahabwa, ulisema ubora wa elimu katika shule unategemea namna zinavyoendeshwa bila ya kukiuka sheria zilizopo.

Anasema baadhi ya shule zinaathiri ufanisi katika utoaji elimu nchini na kwamba maeneo ambayo ukiukwaji wa taratibu unajitokeza zaidi, yanajumuisha ratiba ndefu ya masomo inayoanza alfajiri na kuendelea hadi usiku.


 
Ripoti kadhaa za uchunguzi zilizotolewa na Nipashe mwaka huu kuhusu mada hiyo ikiwamo ya tarehe 3 mwezi huu, ilibainisha kuwapo baadhi ya shule huendesha masomo kwa siku saba za wiki, kati ya Jumatatu na Jumamosi, madarasa yanaendeshwa kwa saa 14, kati ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 4:00 usiku na nyingine zinaishia saa 2:00 usiku.

IIibainika katika ripoti hiyo iliyoonyesha mbinu za kuhadaa wazazi na serikali kutoka shule hizo, kwamba ratiba ya Jumapili maisha ya wanafunzi yanaanzia kanisani asubuhi na mchana wanaingia darasani hadi usiku, kinyume na Sera ya Elimu Tanzania Toleo la 2019, inayoelekeza wanafunzi kusoma kwa siku tano kwa wiki kwa saa zisizozidi nane kila siku.

Mengine anayotaja ni kuzuiwa likizo kwa wanafunzi hususani walio na madarasa yenye mitihani na upimaji kitaifa, pia shule kutoza michango kutoka kwa wazazi au walezi bila ridhaa yao.


Kamishna wa Elimu, ambaye Sera ya Elimu inampa mamlaka makuu ya usimamizi, anafafanua katika waraka wake huo ukiukwaji mwingine unahusu shule kuwapo mazoea ya kufanyika majaribio na mitihani kila mara na hata wanafunzi kupatiwa adhabu kama vile viboko visivyozingatia taratibu rasmi.

Alisema, hiyo inajumuisha suala la viongozi kutoa maagizo kwa shule na kumaliza ufundishaji wa mada zote katika muhula wa kwanza, ili wa pili utumike kwa mazoezi na majaribio, hasa madarasa yenye mitihani na upimaji kitaifa ambayo ni darasa la nne, saba na sekondari kidato cha pili na nne.

“Kutokana na kuongezeka kwa shule zinazokiuka taratibu, wizara inatoa maelekezo haya ili kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo. Kalenda iliyowekwa katika utekelezaji wa mitaala izingatiwe kikamilifu sambamba na nyaraka zote za elimu.

Kimsingi, Sera ya Elimu ya Msingi Toleo la Tatu la Mwaka 2019, inaelekeza mwanafunzi akae darasani kwa siku tano za wiki, ikiwa na jumla ya muda usiozidi saa 30, ikifafanua: “Mwaka wa masomo utakuwa na siku 194 ambazo ni sawa na wiki 39 kwa Darasa la III–VI. Darasa la VII watakuwa na wiki 34 kutokana na darasa hilo kuwa na mtihani wa mwisho mwezi Septemba kila mwaka.


 
Kwa mujibu wa sera hiyo, wanafunzi watasoma vipindi 38 kwa wiki, ambayo ni sawa na jumla dakika 1,520 ambayo ni sawa na saa 25 na dakika 33; hiyo inaangukia wastani wa saa tano kwa kila siku ya masomo, uwiano unaoonyesha wastani wa saa sita uliotajwa kwenye sera, unajumuisha muda wa ziada wa mengineyo kama mapumziko.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad