WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imefanya mabadiliko katika ngazi ya elimu ya msingi kwa kurejesha darasa la saba kuanzia mwaka 2022 kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Simai Mohammed Said amesema mabadiliko hayo ni kwa ajili ya kuimarisha elimu ya msingi kuwa ya miaka saba badala ya sita kama ilivyo sasa.
Waziri Simai amesema kufuatia tathmini zilizofanywa na Wizara pamoja na ushauri wa wadau na wazazi wa Wanafunzi kupitia mijadala mbali mbali wameona kuna haja ya kulifanyia kazi suala hilo kwani Wanafunzi wanaanza elimu ya Sekondari wakiwa na umri mdogo hali inayopelekea matokeo mabaya katika mitihani ya Kitaifa.
Akizungumzia kuhusiana na mabadiliko ya mitaala amesema Wizara ipo katika hatua za kukamilisha mtaala huo kwa ngazi ya maandalizi na msingi ambapo umezingatia mabadiliko mbali mbali ikiwemo kupunguza idadi ya masomo ambavyo yameonekana ni mengi ukilinganisha na uwezo wa watoto katika kujifunza.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar bw Ali Khamis Juma amesema Wizara itatoa muongozo kwa Baraza la Mitihani kupinga matokeo ya Wanafunzi waliofanya mitihani ya darasa la sita kwa mwaka huu ambapo kwa waliofikiwa ufauli wa asilimia 60 ndio watakaoendelea na masomo ya kidato cha kwanza na waliopata asilimia 40 ndio watakaondelea na masomo ya darasa la saba.
Nao baadhi ya Wanafunzi wamepongeza hatua hiyo ya Serikali kwani imeonekana Wanafunzi na wazazi walio wengi walikuwa wakitoa malalamiko yao juu ya watoto wao kupeleka Sekondari wakiwa na umri mdogo ambao bado hawajatambua thamani ya elimu yao.