Zimbabwe Inathamini Mchango Wa Tanzania Katika Ukombozi Wa Taifa Hilo



Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam

Waziri wa Habari na Utangazaji kutoka Jamhuri ya Zimbabwe ambaye pia ni miongoni mwa wapigania uhuru wa taifa hilo Mhe. Monica Mutsvangwa amehitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Desemba 17-19, 2021 nchini kuandaa makala Maalumu ya Ukombozi wa Taifa hillo.


Lengo la ziara hiyo ni kuandaa makala hiyo ya historia ya ukombozi wa nchi hiyo kwa kutembelea maeneo ambayo yalitumiwa na mashujaa wao wakiwa hapa nchini kwa mafunzo mbalimbali ya ukombozi wan chi yao.


Ziara ya kiongozi huyo ilianzia mkoani Dodoma ambapo alikutana na mwenyeji wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ambapo walijadili namna nchi hizo mbili zitanufaika na makala maalum ambayo wanayoiandaa kuhusu historia ya ukombozi wa taifa hilo na namna Tanzania ilivyotoa mchango wake kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.


“Tunathamini mchango wa Tanzania katika ukombozi wa taifa letu, ziara yetu hapa Tanzania ni kuendelea kuimarisha mahusiano kati ya mataifa yetu mawili kuhusiana na maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Zimbabwe, lengo la ziara yetu ni kuandaa makala maalum ambayo itasaidia kuelimisha watu wetu hasa vijana ili kutunza historia yetu isipotee” amesema Mhe. Mutsvangwa.


Amesema kuwa wapigania uhuru akiwemo yeye ambaye alipata mafunzo nchini Msumbiji anawiwa kuhakikisha utajiri huo wa historia ya ukombozi wa taifa hilo isipotee kwa kuwa mashujaa wengi wamekuwa wazee na vijana wengi wamezaliwa hawajui mahusiano ya kidugu yaliyopo kati ya mataifa hayo na hawajui historia ya nchi yao.


Mhe. Mutsvangwa aemsema Tanzania ni nchi ya ya mfano wa kuigwa kwa kuwa ilijitoa kwa hali na mali kusaidia mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Zimbabwe kupitia chama cha ZANU na ZAPU, Angola kupitia chama cha MPLA, Msumbiji kupitia chama cha FRELIMO, Namibia kupitia chama cha SWAPO, Afrika Kusini kupitia chama cha ANC, Zambia kupitia chama cha UNIP na nchi nyingine za Afrika.


Mhe. Mutsvangwa ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa juhudi kubwa inayofanya kutunza utajiri huo wa ukombozi wa Bara la Afrika, kipekee amemshukuru Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka na viongozi wengine wa Serikali ambao wamekuwa mstari wa mbele kufanikisha ziara yao hapa nchini.


Awali akimkaribisha Mgeni wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia Wizara anayoiongoza itatoa ushirikiano kwa msafara wa Waziri huyo wakati wote watakapokuwa nchini ili kufanikisha azama ya ziara hiyo ambayo lengo lake kuandaa makala ya historia ya ukombozi wa taifa hilo katika maeneo yote ambayo yalitumiwa na wapigania uhuru wa nchi ya Zimbabwe wakiwa hapa nchini kwa mafunzo mbalimbali.

“Nchi yetu iliandaa maeneo nchi za kusini mwa Afrika kujiandaa kupigania uhuru wao ikiwemo Zimbabwe, makala hii itasaidia kutunza historia yetu ili isipotee ikiwemo ushuhuda wa wapigania uhuru walioshiriki harakati hizo ambao bado wapo hai na itatoa elimu kwa vijana wetu wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo” alisema Mhe. Bashungwa.


Aidha, Waziri Bashungwa amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ipo mstari wa mbele kutunza utajiri historia ya ukombozi wa Bara la Afrika ambao upo hapa nchini ambapo Programu inayosimamia masuala ya Ukombozi wa Afrika iliyopo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imetengewa fedha na Bunge kupitia bajeti ya Wizara ya Utamaduni, sanaa na Michezo kwa lengo la kutambua, kuhifadhi na kuendeleza utajiri huo wa ukombozi ambao upo hapa nchini.


Maeneo ambayo yalitumiwa na wapigania uhuru wa Zimbabwe hapa nchi yapo Kongwa mkoani Dodoma, Morogoro chuo cha afya, Dar es Salaam kwenye nyumba aliyoishi Rais wa kwanza wa Zimbabwe Hayati Robert Mugabe, Bagamoyo eneo la Kaole, Iringa kwenye kambi ya Mgagao, Nachingwea.


Kwa upande wake mmoja wa wakufunzi wa chuo cha kuwandaa madaktari wa ambacho kilikuwa kinasimamiwa na Umoja wa Mataifa (UN) ambaye pia alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Salum Mwandu amesema lengo la chuo hicho lilikuwa ni kuwahudumia wapigania uhuru wa kusini mwa Afrika ikiwemo Zimbabwe kupitia chama cha ZAPU na ZANU.


“Viongozi wa nchi hizi akiwemo Komradi Mugabe walikuwa wanakuja kuwatembelea wanafunzi madaktari waliokuwa wanasoma hapa na kuonana na mimi ili kupata maendeleo ya wanafunzi wao, hatua hii iliimarisha sana mahusiano yangu na Komradi Mugabe na alinialika mimi na mke wangu mwaka 1982 kusherehekea sherehe za pili za uhuru wa Zimbabwe, najua Uwanja wa michezo wa Rufaru na Mwenemutapa” alisema Dkt. Mwandu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad