Daud Emanuel (27) mkazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro, amenusurika kifo baada ya kumwagiwa mafuta ya petroli kisha kuchomwa moto na rafiki yake aliyefahamika kwa jina la Marko Gerald, baada ya kumtuhumu kuwa anajihusisha kimapenzi na mke wake.
Akisimulia madhira yaliyomkuta huku akiugulia maumivu, Emanuel amesema kuwa tukio hilo limetokea Januari 2, 2022, majira ya saa 3:00 usiku ambapo awali siku ya tukio rafiki yake alimuita nyumbani kwake ili kumsaidia kazi ya kushusha na kupanga magunia ya mkaa.
Emanuel ameongeza kuwa baadae rafiki yake aliondoka na kumuacha na mkewe wakiwa wanamsubiri ili waendelee na kazi aliyomuitia lakini baada ya rafiki yake kuondoka shemeji yake alienda kuoga na alipotaka kubadili nguo alimpisha ili avae na ndipo rafiki yake huyo akarejea na kukuta mkewe akiwa anavaa na kuhisi ametoka kushiriki tendo la ndoa na rafiki yake na ndipo alipomchoma.