NI kitambo, Simba haikuwa na MKuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, tangu alipojiuzulu na kuhamia Jangwani, Haji Manara. Ndio, nafasi hiyo ya Manara ilikaimiwa na Ezekiel Kamwaga kwa muda wa miezi kama miwili hivi kisha jamaa akasepa zake kwenda kusoma.
Kuna majina yalitajwa huenda wangepewa nafsi hiyo. Lakini hakuna shabiki wa Simba aliyewaza jina la Ahmed Ally. Mtangazaji mahiri wa habari za michezo, aliyewahi kutamba ndani ya RFA na Star Tv kisha Azam Media.
Saa chache baada ya kutangazwa kwa uteuzi wake, mitandao ya kijamii ilichafuka. Picha za Ahmed akiwa na mashabiki wa Yanga. Akiwa mbele ya kombe la wakali hao wa Jangwani zikaanza kusambaa kama moto nyikani.
Kuna waliodhubutu kudai kuwa, wanamjua Ahmed kuwa Yanga lialia. Wengine wakadai anazuga kama wanavyozuga wengine kwenye ishu za kazi. Hakuna ubaya katika dunia ya sasa mtu kufanya kazi, maadamu umekithi vigezo na masharti.
Gazeti la Mwanaspoti,lilifanya mahojiano na Msemaji huyo mpya wa Simba visiwani Zanzibar alipo na timu yake inayoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022. Jamaa akafunguka na kulithibitishia Mwanaspoti kuwa yeye ni Mnyama lialia. Haigizi kama wengine na picha zinazosambazwa ni uadilifu wake katika kazi ya uandishi kufanya kazi bila kuendekeza hisia na ushabiki.
Ahmed ameeleza kwa kina zaidi juu ya ajira yake ndani ya Simba na nini kimemsukuma hadi kwenda hapo ambapo amewatoa shaka Wanasimba kuwa wawe na imani naye.
SIO YANGA
Anasema katika miaka 10 ambayo amefanya kazi ya uandishi wa habari hajawahi kujionyesha kama yupo upande gani kwani Simba na Yanga alikuwa akifanyakazi kwa uwiano sawa.
“Kitu pekee nilichofanikiwa katika kazi yangu ya uandishi ni kukwepa kuweka wazi mapenzi yangu ya hizi timu mbili Simba na Yanga. Haya ni mafanikio yangu makubwa sana kwenye kazi yangu
“Ilibaki tu kila mmoja anajiuliza ama kunipeleka upande anaotaka yeye kama mimi ni Simba ama Yanga, hivi ndivyo mwandishi wa habari anatakiwa awe na sio kujionyesha moja kwa moja kuwa upo upande upi kwani utashindwa kufanya kazi yako kwa weledi na kujiondoa kwenye misingi ya taaluma yako.
“Simba na Yanga wanapenda sana vitu vizuri na wanapenda kumiliki hasa mtu anyefanya vizuri hivyo ukitoa nafasi tu basi unaondoka kwenye misingi yako ya kazi ndio maana wengi walikuwa wanaenda kwa hisia tu kuwa Ahmed ni Simba ama Yanga.
“Nimeweza kuishi kwenye misingi ya weledi na kazi ndio maana kwa miaka 10 wameshindwa kunijua mimi ni nani katika timu hizi mbili hata Simba wenyewe walipaga tabu sana kujiridhisha juu ya upande wangu wa timu nao. Walitumia watu wengi kunidadisi na wakati mwingine walinihoji mwenyewe,” anasema Ahmed na kuongeza;
“Hawakuamini moja kwa moja na baada ya kujiridhisha ndio wameamini, ingawa kuna wengine hawajaamini wanajua nimefuata maslahi ila wanapaswa kujua kuwa nimetoka kwenye taasisi imara, madhubuti na kubwa, hivyo isingekuwa rahisi kuacha sehemu ambayo napata nafasi na ninatangaza kazi niipendayo halafu niende sehemu ambayo siipendi.”
“Sasa wanapaswa kutambua kuwa nimeenda sehemu niipendayo na ni timu ambayo naipenda kiukweli sijawahi kuwa Mwanayanga na sidhani kama nitakuwa mwanayanga, mimi ni Mnyama lialia na watu wangu wa karibu wanalijua hili,” anasisitiza.
PICHA ZA YANGA
“Ukiwa mwandishi wa habari unapaswa kuishi katika mazingira ya timu zote ili kazi yako iwe rahisi na kujenga uhusiano mzuri na pande zote hasa hizi timu mbili Simba na Yanga. Ni kweli nilipiga picha na mashabiki wa Yanga tulipokuja hapa Zanzibar kwneye ufunguzi wa Wiki ya Mwananchi isingekuwa rahisi kukwepa hilo.
“Nilipiga nao kama shabiki wao wanayenikubali katika utangazaji jambo ambalo najivunia. Hivyo mashabiki watambue kazi yangu ilikuwa inaniruhusu kuwa rafiki wa wote. Ukifanya kazi na Simba basi unapaswa kuendana na vile tukio lilivyo, hivyo hivyo hata Yanga na ndicho kilichotokea na si vinginevyo kama inavyotafsiriwa sasa,” anasema.
PRESHA YA SIMBA
Anasema ni klabu yenye presha kubwa ndani na nje ya uwanja, hivyo ni wakati wake wa kukabiliana nalo.
“Nimekutana na presha kubwa kabla sijaenda Simba ingawa siwezi kuzilinganisha na presha za klabu hii, sijui presha itakujaje ila nimejipanga kwenda nazo sawa.
“Katika mazungumzo yangu na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez alinishauri hilo pia namna ya kuishi na kuzibeba presha za Simba, ni kwamba ndani ya Simba kuna makundi tofauti ya watu na wenye akili tofauti ambao wote kwa pamoja wakiamua kukupa presha akili zao zinakuwa kama wehu. Hivyo nipaswa kuwa na akili ya afya ili nitulie,” anasema Ahmed na kuongeza; “Nafahamu Simba wanachokitaka hivyo jitajitahidi kuwapa kile wanachokitaka kwa weledi pasipo kuvuka mipaka kwa kukiuka maadili yangu ya kazi japo, ni watu wanaohitaji vitu vilivyochangamka, naamini nitakuwa mtu bora siku zijazo.”
MIPANGO YAKE
“Nimesoma Mass Communications ambayo ndani yake kuna Uandishi wa Habari na Public Relations (Uhusiano wa Umma), ndoto yangu ilikuwa nifanye kazi ya uandishi wa habari kwa miaka 5, lakini nimefanya 10 baada ya kunogewa, kwani napenda sana kutangaza tena kwenye televisheni na sio redio.” “Nililiacha njiani lengo langu ambalo ndiyo hili, lengo hasa ilikuwa ni kufanya kazi kwenye taasisi kubwa za kisoka na kuna wakati niliwahi kuomba kazi hiyo pale TFF nilimweleza Katibu Mkuu Wilfred Kidao, kuwa ikitokea basi anipe nafasi ili nifanye kila ninachokipenda ila haikuwa rahisi.
“Naamini nipo sehemu sahihi sasa ya ndoto yangu kwani Simba ni taasisi kubwa kama nilivyotaka kwenye ndoto zangu huko nyuma kabla sijanogewa na utangazaji.”
UTANGAZAJI NDIO BASI
Anasema anatamani siku moja arudi kwenye kazi aliyoifanya kwa miaka mingi lakini sasa haitawezekana.
“Ninatamani kurudi tena ila sidhani kwani najua sasa sitapendwa tena, nimepoteza imani na mashabiki wa Yanga hawatatamani kuniangalia tena nikichambua michezo. Kiweledi inatia ukakasi sana sasa watanichukia na hawatanipenda tena.
“Maisha yamenipeleka huku ingawa nitaikumbuka sana kazi yangu, nitakumbuka mno kutangaza mbele ya kamera lakini sina namna kurudi huko kama nilivyosema kuwa sio jambo rahisi tena. Sasa napaswa kuishi kwa misingi hii ya ndoto yangu,” anasema
UJUMBE MWEZI MZIMA
“Haijawahi kutokea kupokea simu ama ujumbe wa meseji kwa kiasi hiki. Kifupi hadi sasa sijamaliza kusoma meseji za watu nahisi itanichukuwa hata mwezi mzima hivyo naomba watu tuvumiliane kwani napokea meseji na simu nyingi sana.
“Nilijitoa kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp lakini nimejikuta nimeingizwa kwenye makundi ya Simba zaidi ya yale niliyokuwa nayo awali. Huu wote ni upendo na wanaonyesha wananikubali kuwepo ndani ya Simba inanipa faraja,” anasema Ahmed.
AIONA WAPI SIMBA
“Simba imepiga, hatua ingawa msimu huu ni kama kidogo mambo sio mazuri ingawa sio ya kutupa presha ni ya kiufundi na yanarekebishika. Tutakuwa bora zaidi,” anasema Ahmed aliye amevitumikia vyombo viwili pekee Sahara Media na Azam Tv tangu ahitimu uandishi.