Mbeya. Aibu! Ndivyo unaweza kusema baada ya Tanzania Prisons kuaibishwa nyumbani kwa kushushiwa mvua ya mabao dhidi ya Azam kwa kulala na kipondo cha 4-0.
Kipigo hicho kinakuwa cha pili mfululizo baada ya mechi iliyopita kufa kwa mabao 2-0 dhidi ya KMC na leo tena ikiwa uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga imekubali kushonwa mabao hayo bila majibu.
Huu ulikuwa mchezo wa pili kwa Kocha wake raia wa Kenya, Patrick Odhiambo ambaye ameanza kwa shubili kazi yake kwa Maafande hao.
Kipigo hicho kizito kinakuwa cha pili kwenye rekodi ya timu hiyo kwani waliwahi kuchakazwa mabao 3-0 wakiwa Sumbawanga dhidi ya Biashara United, walipokuwa chini ya Salum Mayanga aliyetimkia Mtibwa Sugar.
Katika mchezo wa leo Jumamosi, Azam ilionekana kutulia na kucheza soka safi na la mipango na kuweza kunufaika zaidi na matokeo hayo.
Tepsi Evance ndiye aliitanguliza Azam dakika ya 28 lililodumu hadi mapumziko huku wenyeji walipambana kusawazisha bila mafanikio.
Kipindi cha pili ndicho kilikuwa cha zahma zaidi kwa Tanzania Prisons baada ya kujikuta ikiruhusu mabao matatu na kuwafanya Wajelajela hao kuondoka kimya uwanjani hapo.
Mabao mengine yaliyokamilisha idadi hiyo yaliwekwa wavuni na Ismaili Kader dakika ya 68, Ibrahim Ajibu dakika ya 71 na Charles Zullu dakika ya 83 na kuihakikishia pointi tatu Azam FC.
Ushindi kwa matajiri hao wa Dar es Salaam unakuwa wa pili mfululizo ugenini chini ya Kocha wake, Abdihamid Moalin baada ya awali kuwanyoa Mbeya Kwanza bao 1-0 na kujikusanyia alama sita ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na kupanda hadi nafasi ya nne kwa pointi 21.