Katavi. Edmond Sungura (53) mkazi wa mtaa wa Rungwa kata ya Kazima Manispaa ya Mpanda amekutwa amejinyonga hadi kufa chumbani kwake kwa kutumia kamba ya viatu vyake.
Akizungumza na mwananchi leo Januari 05,2022 mke wa marehemu Astilida Makambila amesema waligundua tukio hilo saa 2:00 asubuhi baada ya kumuamsha pasipo mafanikio.
Amesema Januari 2, 2022 saa 2:00 usiku marehemu alitoka kunywa pombe akiwa amelewa alifika nyumbani na kumuita mke wake chumbani kisha kumkabidhi simu mbili.
“Aliniambia chukua simu ziweke mezani hii moja ni ya rafiki yangu nimeona amechoka sana ataijia asubuhi,nikazichukua nikaenda sebuleni kuangalia TV na watoto,”amesema Astilida akaongeza.
“Akatoka chumbani akasema naomba muondoke mtoke nje akazimisha TV tukatoka,akatufuata akasema hapa ndiyo nje?naomba mtoke nitawachafua,"
Amesema walitoka nje wakakaa barabarani ilipofika saa 6:00 usiku walirudi kwenda kuangalia kama amelala walikuta mlango umefungwa ikabidi walale chumba kingine.
“Asubuhi tuliamka nikamuita baba Tedi kimya, nikachukua panga nikachana wavu wa dirisha nikachungulia nikamuona amening’inia kwenye paa la nyumba nikaenda kuwaita viongozi,”
“Alikuwa na tabia ya kutishia kujinyonga mara kwa mara akiwa amelewa nilikuwa nawaeleza ndugu zake na viongozi,”
Mwenyekiti wa mtaa huo Mwelela Nkokwa amekiri kupokea taarifa za tukio hilo na kwamba alipigiwa simu na balozi wake akiwa anatoka kanisani.
“Aliniambia kuna mtu amejinyonga nikaenda nikashuhudia amejitundika na kamba ya viatu, nikapiga simu polisi wakaja tukahojiana,”
“Niliwaeleza ni zaidi ya mara tatu anataka kujinyonga akiwa amelewa, mke alikuwa anakuja kulalamika,kwenye mtaa wangu ni mtu wa pili kujinyonga,”amesema Nkokwa.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Katavi ACP Ally Makame amethibitisha kutokea matukio ya watu wawili kujinyonga kwa wakati tofauti.
“Sungura amejinyonga kwa kamba ya viatu chanzo chake ni ugonjwa wa afya ya akili,Ndebi Samweli (35) mkazi Kasinde amejinyonga kwa kamba ya manila kwenye mti wa mwembe chanzo ni wivu wa kimapenzi,”amesema Makame.