Jeshi la Polisi mkoa wa mtwara limewafikisha maafisa saba wa Jeshi hilo katika Mahakama ya Hakimu Hakimu Mkazi Mtwara, kwa tuhuma ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis aliyekuwa akiishi Nachingwea mkoani Mtwara.
Miongoni mwa washtakiwa hao ni Gilbert Kalanje, ambaye aliwahi kumtolea bastola Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye.
Tukio la Nape kutishiwa kwa bastola lilitokea Machi 23, 2017, baada ya mwanasiasa huyo kutenguliwa katika wadhifa wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alipokuwa akijiandaa kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Maofisa wengine waliotajwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera ni aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango, aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia Mkoa, Mrakibu wa Polisi, Bicolas Kisinza, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Mbota, Mkaguzi wa Polisi, Shiraz Ally Mkuka na G5158, Koplo Salum Juma Mbalu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lugano Kasebele alisema washtakiwa walifikishwa mbele yake na kusomewa mashtaka, lakini hawakutakiwa kujibu chochote.
“Upelelezi bado haujakamilika, hivyo kesi hiyo itatajwa tena Februari 8, 2022. Upelelezi utakapokamilika kesi hiyo itapelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Kusini kwa ajili ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Kasebele.
Aliongeza kuwa kwa kuwa shtaka walilosomewa halina dhamana, washtakiwa hao wamepelekwa rumande katika gereza la Lilungu lililopo wilayani Mtwara.
Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wilbroad Ndunguru.
Hata hivyo, miongoni mwa maofisa wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo, alikuwa Grayson Mahembe anayedaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa mahabusu, jambo lililozua maswali kuhusu uwezekano huo huku familia yake ikitaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili haki iweze kutendeka.