IKIWA imepita wiki moja na nusu tangu mkazi wa Kijiji cha Msikisi, wilayani Masasi, Ayuba Mawazo (26), kutolewa taarifa kuwa amefariki dunia na baadaye kuzinduka, mauti yamemfika na kuzikwa jana kijijini kwao.
Desemba mwaka jana, Mawazo alitolewa taarifa kutoka kwa baadhi ya familia yake kuwa amefariki dunia akiwa njiani kutoka Hospitali ya Mkomaindo Masasi alikolazwa na wanakijiji kukusanyika nyumbani kwake kwa ajili ya shughuli za mazishi, lakini muda mchache baadaye familia ilitoa taarifa kuwa ndugu yao alikuwa amepoteza fahamu.
Akithibitisha kifo hicho baba mzazi wa marehemu, Mawazo Awadi, alisema kijana wake alifariki dunia jana saa 11 alfajiri nyumbani akipatiwa matibabu ya tiba asili baada ya hospitali kushindikana.
Alisema hali yake ya kiafya iliendelea kuwa mbaya.
Awadi alisema mwezi Desemba mwaka jana, Ayuba alianza kuugua ghafla na familia kwa shirikiana naye waliamua kumpeleka Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Masasi Mkoamiando kwa ajili ya matibabu zaidi.
Alisema alipofanyiwa vipimo aligundulika na tatizo la kiwango kidogo cha sukari katika mwili wake (Hyporglycemia) ugonjwa ambao ulionekana kumsumbua kwa muda mrefu mpaka umauti unamkuta.
Alisema awali, wanafamilia walipoona hali ya kijana wao ikiendelea kuwa mbaya hospitali waliamua kumtoa na kurudi naye nyumbani na kuangalia njia mbadala ya kumpatia matibabu ambayo sehemu kubwa ilikuwa ni matibabu ya kiasili hadi anafariki dunia.
Alisema kutokana na awali kuwapo taarifa zilizoibua taharuki kuhusu mtoto wake kutangazwa kufa na kuzinduka ghafla, sasa ameamua pia kutoa taarifa rasmi kwamba mwanawe amefariki dunia baada ya kuumwa kwa muda wote huo na kuzikwa rasmi jana katika makaburi ya kijijini hapo.
“Ni kweli ndugu yetu amefariki dunia alfajiri hii ya leo (jana) na ilipofika saa nane mchana tumeamua kufanya mazishi na taratibu zote zinazopaswa kufanyika tunawashukuru wananchi wote hapa, kwa kutukimbilia kwa ajili ya mazishi ya ndugu yetu huyu,” alisema Awadi.