Askari Aliyemuua Baba Yake Alipomaliza Alisema "Nimemaliza Kuchinja Kuku”

 


Mussa Edward Ndonde, Mtumishi wa Jeshi la Kujenga Taifa, Ruvu JKT, anaedaiwa kufanya mauaji ya baba yake mzazi siku ya Jumatano Januari 12, 2022 nyumbani kwa baba yake mtaa wa Lumbira Kata ya Iwambi jijini Mbeya, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi wakati uchunguzi ukiendelea.


Mauaji haya ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Edward Ndonde anayedaiwa kuuawa kikatili kwa kuchomwa visu yalithibitishwa na JESHI la Polisi mkoani Mbeya ikielezwa kuwa ni sababu ya kutuhumiana kwa mambo ya kishirikina kati ya baba na mtoto.


Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Christina Musyani alisema mtuhumiwa ambaye ni mtumishi wa Ruvu JKT uchunguzi unaendelea ili hatua za kisheria ziweze kushika mkondo wake.


“Ni kweli tukio lipo na limetokea leo, ambapo pia marehemu alikuwa mwalimu msitaafu, chanzo kinadaiwa kuwa mambo ya kishirikina, ambapo mtuhumiwa alikuwa anamtuhumu baba yake kuwa ni mchawi na Jeshi la Polisi limemshikilia kwa uchunguzi zaidi,” amesema Christina.


Habari kutoka kwa mashuhuda zinasema kuwa Mussa baada ya kumuua baba yake alitoka nje na kuongea mneno ambayo yanaashiria kuwa alifanya mauaji kwa kutumia kisu.


“Nimemaliza kuchinja kuku”. Ni kauli ya Mussa Edward, ambapo mashuhuda wakiongea na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, walisema mauaji hayo hayakuchukua muda mrefu na walipokuja kuona walikuta damu zimetapakaa ndani na mtu ameshafariki.


Alex Mwang’ande ambaye ni jirani kwa marehemu, alisema alishtushwa na taarifa hizo, kwani kabla ya tukio hakufahamu mapema kilichokuwa kinaendelea hadi aliposikia kelele zikitoka ndani ya nyumba marehemu.


Alisema baada ya kelele hizo, alifika nyumbani kuona kinachoendelea, “Baada ya kuingia ndani mama yake na mtuhumiwa akawa analia kwa uchungu, huku mtuhumiwa akisema amemaliza kuchinja kuku, tunakuja kuangalia vizuri tukakuta damu zimemtapakaa sehemu za mikononi hadi mwilini,”


“Hapo nilikuwa na balozi wa mtaa, tukaamua kuingia ndani kuona huyo kuku aliyechinjwa tukakuta tayari ni baba yake ameshakufa tayari akiwa majeraha kutokana na kuchomwa kisu ambacho kilikuwa kimevunjika kimetupwa pembeni,” alisema Mwang’ande.


Aliongeza kuwa mbali na tukio hilo, mtuhumiwa na baba yake walikuwa na ugomvi wa muda mrefu kwani ni zaidi ya mara moja amewahi kuamua ugomvi wao kwa vipindi tofauti.


Aliongeza kuwa baada ya wananchi kuona unyama huo, walimvaa mtuhumiwa na kuanza kumpa kichapo, ambapo aliingilia kati na kuita Jeshi la Polisi ambalo liliweza kumchukua.


Kwa upande wake, Balozi wa Mtaa huo, Hezron Thobias alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 4 asubuhi, akiwa anatoka kwenye shughuli zake alikuta taarifa mtaani kwake wakimueleza kilichotokea kwa marehemu.


Balozi Hezron alisema katika kumchunguza mtuhumiwa walibaini alikuwa ameweka ugoro mdomoni akionekana kuwa amelewa, huku akieleza kuwa wawili hao hawakuwa na maelewano mazuri kwa kipindi cha nyuma.


Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Alhaji Saad Kusilawe alisema marehemu alikuwa mtumishi mwenzao kwenye chama kabla ya kustaafu.


“Ni mshtuko na pigo kubwa kwani ameacha pengo na ni masikitiko kwani alikuwa mashuhuri na tulihitaji zaidi busara zake, lakini tunakubaliana na kilichotokea na nitoe pole kwa ndugu, jamaa na ndugu na chama kwa ujumla” alisema Kusilawe.


Katika uhai wake Marehemu, aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wazazi Taifa hadi anastaafu na alikuwa mwadilifu katika utumishi wake na alikuwa kama hazina katika kutoa ushauri kwa vijana wanaochipukia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad