MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imeharibu nyumba 45 katika mtaa wa kineng’ene , kata ya Mtanda manispaa ya Lindi.
Imeelezwa kuwa kutokana na hali hiyo, wakazi hao kwa sasa wamekosa makazi, huku diwani wa kata hiyo, Abedi Abedi, akisema kuwa tukio hilo lilitokea na kusababisha hasara ambayo bado haijafahamika.
Abedi amesema mvua iliyoambatana na radi na upepo mkali ilibomoa nyumba saba, huku 38 kikiwamo kituo cha afya zikiezuliwa paa na kusababisha taharuki kwa jamii, wakiwamo wagonjwa waliofika kupata huduma za matibabu.
“Hadi tunapoongea na wewe majengo yaliyobomolewa na mvua ni 45 kikiwamo kituo chetu cha afya,” alisema Diwani Abedi.
Diwani huyo amefafanua kuwa nyumba 38 kikiwamo kituo cha afya zimeizuliwa paa, wakati saba zilizojengwa kwa kutumia miti na udongo zinazokaliwa na wazee wasio na uwezo na wenye ulemavu zimeanguka kabisa.
Alisema kufuatia tukio hilo, mmoja wa wakazi hao aliyemtaja kwa jina la Chautite alijeruhiwa kwa kukwaruzwa na bati eneo la taya wakati akijaribu kujiokoa kutoka ndani ya nyumba yake iliyokuwa imeezuliwa paa.
“Kwa sasa waathirika hawa wanahifadhiwa kwa majirani ambao nyumba zao zimenusurika,” alisema Diwani Abedi. Alibainisha kuwa taarifa ya tukio hilo, imeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Juma Nnwele, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, ili kufanya tathmini itakayotoa thamani halisi ya hasara iliyopatikana.
Haji Makupula, mkazi wa mtaa huo akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema licha ya kuezua mapaa na kubomoa nyumba, mvua hiyo iliharibu vyakula kama unga, mchele na sukari.
Alisema kituo cha afya Bati kiliezuliwa choo na kliniki, hivyo kusimamisha utoaji huduma kwa wagonjwa.
Mwandishi alipowasiliana na Nnwele kupitia simu yake ya mkononi, alijibu yupo safarini na kumtaka kwenda kuonana na aliyemwachia ofisi, Dk. Danford Mwaitege, lakini naye alisema amekwenda kata ya Mnazi Mmoja kikazi.
NYUMBA 16 ZAEZULIWA
Kaya 16 katika Mtaa wa Kasanga, Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro, zimekosa makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa paa na upepo mkali usiku wa kuamkia jana.
Akizungumza na Nipashe Diwani wa Kata ya Mindu, Zuberi Mkalaboko, alisema upepo huo ulianza kuvuma kwa kasi majira ya saa tano za usiku ukiambatana na mvua kubwa.
Alisema athari nyingine zimejitokeza katika Shule ya Msingi Kasanga baada ya kisima kinachotumiwa na shule hiyo kubomoka na baadhi ya miundombinu.
“Nyumba zilizoezuliwa nyingi ni zile ambazo watu walikuwa wanaishi na baadhi ya nyumba ambazo hazijamalizika, lakini kikubwa tunaomba misaada ya kibinadamu kama chakula na malazi kwa kipindi hiki katika kuwasitiri ndugu zetu,” alisema.
Alisema tayari hatua za awali za kukabiliana na janga hilo zimeanza kuchukuliwa ikiwamo kutoa taarifa katika serikali ya wilaya na kamati ya maafa huku wadau mbalimbali wakianza kutoa misaada.
Kelvina Mshana, mmoja wa waathirika katika tukio hilo, alisema wakati nyumba yao inaezuliwa walikuwa wamelala na watoto ndani na kulazimika kukimbia kuomba hifadhi kwa jirani yao.
Aliomba serikali kuwasaidia ukarabati wa nyumba zao na chakula kwa kuwa akiba za vyakula vyao vimeingia maji na kuwaacha wakiwa hawana mahali pa kujihifadhi.
“Wakati mvua inaanza kunyesha tulienda kulala tukijua ni ya kawaida baadaye ndiyo ukaja upepo mkali na kuezua paa ya chumba tulichokuwa tumelala ikabidi tuamke tutafute sehemu iliyo salama ndipo tukaona nyumba nzima imeezuliwa na upande mmoja wa ukuta ukaanguka,” alisema.