WATU wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa kufuatia ajali ya lori lililovamia kituo cha daladala cha Kimara Suka jijini Dar es Salaam leo Januari 28, 2022.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Usalama wa Barabarani Taifa, ACP Abdi Isango amefika eneo la tukio, lakini amesema hawezi kutoa taarifa mpaka atembelee hospitali zote ili ajuwe idadi ya majeruhi na waliopoteza maisha.
Mashuhuda wa ajali hiyo wameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo gari hilo lilionekana kupoteza mwelekeo baada ya kufeli breki na kuwapitia watembea kwa miguu waliokuwa eneo hilo hivyo kusababisha vifo vyao na majeruhi.
“Mimi nimesimama pembeni naona gari linanifuata na lilikuwa katika spidi kubwa sana niliruka mtaroni ndicho kilichonisaidia bila hivyo sijui,” amesema John Kelvin aliyekuwa amepaki boda boda yake pembeni.
“Rafiki yangu mshtuko alikimbia mbio limemkuta huko huko nikamuona anaingia chini ya lori ndio wamemtoa ameshakufa jamani,” amesema.
Mmoja wa ndugu wa majeruhi ambaye hakuta jina lake kuandikwa gazetini amesema amefuatwa nyumbani na boda boda akaambiwa mke wake Aisha amekatika sikio.
“Nilitoka nyumbani haraka sana, nilikuwa mke wangu amewekwa kwenye Kirikuu nikamtoa nimeleta mwenyewe hapa Bochi nikasaidia na wengine wawili.
“Ajali ni mbaya jamani maana imewafuata watu pembeni mimi mke wangu alikuwa anaenda kazini jamani hali yake sio nzuri,” amesema.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne Muliro amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema jeshi hilo linamsaka dereva aliyesababisha ajali hiyo.