Watu tisa wamefariki dunia, sita kuokolewa wakiwa hai na wengine zaidi ya kumi hawajulikani walipo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama baharini huko Mkoa wa Kusini Pemba. Zanzibar.
BBC imezungumza na kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Pemba Richard Thadei Mchomvu ambaye amethibitisha kutokea ajali hiyo jana jioni wakati watu hao wakitokea Chakechake kwenda msibani katika kisiwa cha Panza.
Kamanda Mchomvu amesema chanzo cha ajali hakijajulikana mpaka sasa ila boti lilikuwa na takribani watu 30 na 40 au zaidi, na mpaka sasa tisa wamefariki dunia wote wanaume watu wazima na sita wapo hai wanapata matibabu.
"Nahodha hajapatikana na hali ya hewa haikuwa mbaya hivyo hatujajua chanzo kamili maana inaonekana tatizo sio upepo,"Kamanda alieleza.
Aidha alisema zoezi litaendelea leo Jumatano asubuhi kufuatilia na jana zoezi lilisitishwa kwasababu ya giza ila ana hakika wote watapatikana wakiwa hai au vinginevyo.
Kwa upande wa idadi ,kamanda anasema utaratibu wa hapo haukuwa na uhakika ila ni takribani watu 30 au zaidi ila idadi kamili haijulikani.