Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amedai kuwa kauli aliyoitoa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, juu ya deni la taifa ni fedheha kwa Rais Samia Suluhu Hassan na uchochezi kwa nchi.
Boisafi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Januari Mosi, 2022 wakati akitoa tamko la chama hicho kwa mkoa huo kuhusiana na kauli hiyo, ambapo amesema kiongozi huyo anapaswa kujitafakari.
"Kauli aliyoitoa Ndugai ni fedheha kwa Rais Samia Suluhu Hassan, matamshi yale ni kama kejeli kwamba nchi inaweza kupigwa mnada, na ile ni kauli ya kichochezi ndani ya nchi yetu, kwa kuwa mama (Rias Samia Suluhu) ameitendea haki Serikali, kwani katika kipindi cha miezi tisa kila mtu ameshuhudia kilichofanyika na mambo mazuri yaliyoko mbele yanafurahisha" amesema Boisafi.
ccm pic1
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi akitoa tamko la chama hicho kwa mkoa huo kuhusu kauli aliyoitoa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, juu ya deni la taifa
Boisafi amesema katika utaratibu mzima wa mkopo wa masharti nafuu wa Sh 1.3 trilioni, Bunge lilikaa wakaona ni namna gani fedha hizo zitumike kuleta maendeleo yatakayowagusa wananchi wote na baada ya hapo Rais aliita Halmashauri kuu ya chama hicho na viongozi wa mikoa kutoa muelekeo wa fedha hizo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec) Mkoa wa Kilimanjaro, Seleman Mfinanga amesema Rais Samia amefanya mambo makubwa katika kipindi kifupi na alishirikisha kila jambo alilotaka kulifanya na watanzania wote wanapaswa kumuunga mkono na kujivunia mafanikio yaliyopatikana.
Akizungumza hivi karibuni katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma, Ndugai alitetea uamuzi wa Bunge kuanzisha tozo za miamala ya simu, kuliko kuendelea kukopa.
"Juzi mama ameenda kukopa 1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alisema Spika Ndugai.
"Tutembeze bakuli ndio heshima, tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku,’ amesema Ndugai huku akitetea tozo kwamba;
“Tukasema pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.
“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya ku-run nchi (kuongoza nchi) hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” alihoji Ndugai.