Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka akitangaza mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kumpata mwanachama atakayewakilisha chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.
Unguja. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza ratiba ya kuchukua na kurejesha fomu za kumpata mwanachama atakayewakilisha chama hicho kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.
Hatua hiyo inakuja baada ya aliyekuwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo Januari 6, 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Januari 9 katika ofisi Kuu za CCM Kisiwandui Zanzibar, Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema mchakato wa kuchukua fomu utaanza Jumatatu Januari 10, 2021 na mwisho wa kurejesha itakuwa Januari 15, 2022.
Shaka “Kuanzia Januari 10 hadi 15 zitakuwa siku za uchukuaji na urejeshaji fomu hivyo wanaCCM wenye sifa wafike makao Makuu ya Chama Dodoma, Ofisi ndogo Lumumba na Kisiwandui Zanzibar”. amesema nakuongeza “Utaratibu huo ni kwa mujibu katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inayotambua spika kuwa ni kiongozi mkuu wa Bunge na nafasi hiyo haiwezi kuwa wazi na bunge likaendelea kufanya shughuli zake,” amesema Shaka.
“Katika kutekeleza matakwa hayo CCM inatangaza rasmi mchakato kujaza kiti sambamba na vikao vya mchujo na uchaguzi wa wabunge wa CCM kabla ya kupelekwa bungeni kupigiwa kura,”
Amesema baada ya wanaotaka kuwania nafasi hiyo kurejesha fomu, Januari 17 sekretarieti ya halmashauri kuu ya Taifa itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa juu ya wagombea waliojitokeza.
Januari 18 hadi 19 kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho ambapo kamati kuu ya halmashauri kuu itafanya kazi hiyo.
Amesema kuanzia Januari 21 hadi 30 wabunge wa CCM watapiga kura kumpata mtu atakayekwenda kusimama bungeni kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa kuwa Spika wa Tanzania.
Amesema fomu zitatolewa Makao Makuu Dodoma, Ofisi Ndogo Lumumba Dar es Salaam na Afisi Kuu Kiwandui Zanzibar kwa gharama ya shilingi milioni moja.