Chama Afunguka "Nimerudi Nyumbani"



WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco akiwapongeza wachezaji wake kwa kufuta historia ya kupoteza mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, kiungo Mzambia Clatous Chama amesema amerejea nyumbani.

Simba ilimtangaza rasmi Chama amerejea kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana akitokea RS Berkane ya Morocco ambayo ilimnunua kiungo huyo mwaka jana.

Chama, nyota anayekipiga pia katika Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo), alisema anaamini ujio wake utaisaidia Simba kufikia malengo kwa sababu kwa sasa uwezo na uzoefu wake umeongezeka.

"Mwenda kwao si mtoro," alisema kwa kifupi Chama baada ya kutangazwa amerejea Msimbazi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah, aliliambia gazeti hili wamejipanga kuendelea kuiimarisha timu hiyo ili ifanye vizuri zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, michuano ya Kombe la FA na mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika wanayoshiriki.


Salim alisema wamefanya usajili huo kwa kuzingatia mahitaji halisi na ripoti iliyowasilishwa na benchi la ufundi la timu hiyo pekee nchini iliyobakia kwenye michuano ya kimataifa.

“Mashabiki wanatakiwa kuwa watulivu kwa sababu ndani ya hizi siku mbili tutaweka wazi usajili tuliofanya katika dirisha dogo, lakini pia tumeweka mipango yetu sawa kuhakikisha tunafanya vizuri katika kila michuano iliyopo yetu,” alisema kiongozi huyo.

Alisema timu yao imekuwa na mabadilko makubwa na wachezaji wanacheza mpira 'biriani' ambao walikuwa wakicheza msimu uliopita.


Akizungumza gazeti hili jana, Pablo alisema anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana katika muda wote wa mechi hiyo ya fainali na hatimaye kutimiza malengo yao ya kulichukua kombe hilo mwaka huu.

Pablo alisema mchezo ulikuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa, lakini pia anawapongeza wachezaji wa Azam FC kwa kucheza mpira mzuri ambao lengo lake ulikuwa ni kupata matokeo chanya ambayo kwao yalikosekana.

“Sasa tumemaliza Mapinduzi na tunarejea katika Ligi Kuu, tutahakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu ijayo kwa kucheza soka safi kama ilivyokuwa kwenye michuano ya Mapinduzi,” alisema Pablo.

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ambaye aliibuka Mfungaji Bora wa mashindano hayo alisema anafurahi kupata tuzo hiyo na kuongeza si uwezo wake binafsi bali ni ushirikiano mzuri alioupata kutoka kwa wachezaji wenzake wa timu hiyo.


Kagere alisema kazi yake kubwa ni kufunga na ataendelea kufanya hivyo kila atakapopata nafasi ili kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine inayowakabili.

“Tumemaliza Mapinduzi, sasa akili na nguvu zetu zote zinaelekezwa katika Ligi Kuu, tunaenda kupambana ili kupata matokeo mazuri katika kila mechi tutakayocheza,” alisema Kagere.

Tayari mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi wamesharejea Dar es Salaam tangu jana na wanajipanga na leo wanaanza mikakati ya kuelekea Mbeya kwa ajili ya kukutana na Mbeya City hapo keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya.

Mbali na kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, tuzo nyingine zilizochukuwa na nyota wa Simba ni ya Mchezaji Bora wa michuano hiyo ni Pape Sakho, Golikipa Bora ni Aishi Manula na Mchezaji Bora wa mechi ya fainali ni Henock Ibanga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad